ZEC yaonya mihemko ya kisiasa wasimamizi wa uchaguzi, wasiegemee upande

Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi kujiepusha na mihemko ya kisiasa, badala yake wasimamie misingi ya maadili wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 17, 2025 na Kamishna wa Tume hiyo, Awadh Ali Said, wakati akifunga mafunzo ya siku tano kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa majimbo yote 50 ya Zanzibar yaliyoanza Agosti 12, ikiwa ni safari ya kuelekea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Ametumia fursa hiyo pia kuwakumbusha maofisa wakati wa kutoa huduma za uchaguzi bila ya kuegemea upande   wa chama chochote cha siasa au kufuata maagizo ya mtu au kundi lolote la ndani au nje ya nchi.

“Nataka niwasisitize wasimamizi wasaidizi wa majimbo yote ya uchaguzi katika kutekeleza majukumu yenu mwende mkasimamie maadili, kila mwenye haki ya kupiga kura aitekeleze bila kikwazo na tujiepushe na mihemko ya kisiasa, kwani kufanya hivyo ni kukengeuka na kukiuka sheria na maadili ya kazi zetu,” amesema Kamishna Awadh.

Kamishna huyo amewakumbusha kwamba uchaguzi ni tukio moja linalokutanisha watu mbalimbali kwa wakati mmoja hivyo wajitahidi kutoa huduma bora na matumizi mazuri ya lugha  kwa wananchi watakaofika vituoni kupiga kura..

“Nimeamua kuyasema haya kwa sababu kumekua na malalamiko katika chaguzi zilizopita, kuna baadhi ya watendaji kukosa nidhamu ya kazi kwa wataka huduma, kwa vile nyinyi mmepikwa vyema kwa muda wa siku tano kwa kupata dozi ya nadharia na vitendo pamoja na maonyeshombinu.

“Hatutegemei kutuangusha katika eneo hili na mtakwenda kutimiza wajibu wenu na kuiheshimisha Tume,” amesema.

Pia, amewataka kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu na watu wenye ulemavu watakapojitokeza kutaka huduma na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwani wana haki sawa na wengine.

“Kwa hiyo lazima watu hawa wapewe kipaumbele katika maeneo yote kulingana na mahitaji yao kwenye mchakato mzima, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeitendea haki sera yetu ya jinsia na ushirikishwaji wa makundi maalumu ya kijamii ya mwaka 2015.

Naye Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina, ameahidi kuendesha uchaguzi huru, haki na salama kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Kwa upande wake Ofisa uchaguzi Wilaya ya Kaskazini B,  Maryam Majid Suleiman, ameahidi kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2025 unafanyika kwa amani na utulivu na kila mwenye haki anaipata. 

Naye Msaidizi msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Chaani, Omar Khamis Haji amesema mafunzo hayo yamewapa mwelekeo wa namna ya kusimamia uchaguzi, kutoa mafunzo kwa washiriki wote wa uchaguzi ikiwemo watendaji wasaidizi, mawakala na wadau wengine.