10 mbaroni wakidaiwa kupanga njama za uhalifu

Kibaha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watu 10 wanaodaiwa kupanga njama za kufanya uhalifu katika Wilaya ya Kibaha, kufuatia taarifa za kiintelijensia zilizopatikana Jumamosi Agosti 16, 2025.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase leo Jumatatu Agosti 18, 2025, hatua hiyo ilichukuliwa baada ya jeshi hilo kupata fununu za uwepo wa mkutano wa siri uliofanyika kwenye moja ya kumbi za sherehe katika eneo la Mailimoja Shule, washukiwa hao walihusishwa na mipango ya kihalifu.

Amesema watuhumiwa hao wanatokea Moshi mkoani Kilimanjaro,Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha.

Kamanda Morcase amesema jeshi hilo linafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi, kuhakikisha maisha na mali za wananchi zinalindwa.

“Kukamatwa kwa watuhumiwa hawa ni sehemu ya jitihada zetu za kudhibiti uhalifu kabla haujaleta madhara kwa jamii,” amesema kamanda huyo.

Wakizungumza na Mwananchi kuhusu taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, baadhi ya wakazi wa Kibaha akiwamo Rehema Mushi, amepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Polisi.

“Kwa kweli tunafarijika kuona polisi wanachukua hatua mapema. Hii inatupa amani ya kuendelea na shughuli zetu za kila siku bila hofu,” amesema mkazi huyo.