Aisha Masaka kutimkia Hispania | Mwanaspoti

Mshambuliaji wa Brighton, Aisha Masaka huenda akatolewa kwa mkopo au kuuzwa moja kwa moja katika moja ya timu za Ligi Kuu ya Wanawake Hispania msimu ujao kama watafikia makubaliano ya ofa.

Mwanaspoti inafahamu mshambuliaji huyo wa timu ya taifa, Twiga Stars, amebakiza mkataba wa mwaka mmoja England kati ya miwili na utamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti moja ya sababu ni kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza na kinachowashawishi zaidi ni ofa mbili alizonazo kutoka Ligi Kuu Hispania.

“Bado ana mkataba wa mwaka mmoja, kama timu zitaweka mkwanja mrefu anaweza kuuzwa moja kwa moja au kama haitaridhiwa anaweza kusubiri hadi mwishoni mwa msimu huu,” alisema mtu huyo na kuongeza;

“Lakini Brighton wanaangalia sehemu bora zaidi kwake kucheza na kukua kwa sababu wanaamini ni mchezaji mzuri na bado mdogo, ndiyo maana kuna machaguo mawili, hapo wanaangalia kwa ukaribu.”

Msimu uliopita nyota huyo wa zamani wa Yanga Princess alicheza mechi mbili pekee kwa dakika 14.

Masaka kabla ya kujiunga na Brighton aliwahi kuichezea BK Hacken ya Sweden akicheza mechi 14 na alifunga mabao matano.