OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema katika jezi yake ataandika jina la kiungo wa Taifa Stars, Yusuph Kagoma ili kumhamasisha afanye vizuri mechi ya robo fainali dhidi ya Morocco kwenye Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Agosti 22 mwaka huu, Taifa Stars itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar kumenyana na Morocco ukiwa ni mchezo wa robo fainali wa michuano hiyo utakaochezwa saa 2:00 usiku.
Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo Agosti 18, 2025 jijini Dar, Kamwe amesema atafanya hivyo ili kumpa hamasa Kagoma afanye kazi ya ziada kwenye eneo la kiungo cha kati.
“Kagoma anapofanya vibaya kila mmoja anazungumza lake mitandaoni, sasa hivyo inamtoa mchezoni, kiukweli nitaandika jezi yangu jina la Kagoma,” amesema Kamwe na kuongeza.
“Asiogope kadi tena na wale Morocco afanye kazi ya kukata kwa sababu kazi ya kiungo wa kati ni kazi kweli kweli sio ya kawaida.”
Mbali na hilo, Kamwe amewataka mashabiki kutoihofia Morocco akiamini Stars ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri.
“Kwa mujibu wa takwimu Stars ndio timu iliyoruhusu mabao machache na imetinga hatua hii bila kupoteza mechi yoyote, kwenye tuzo tumebeba zote, kiufupi viwango vya wachezaji wetu ni vikubwa, sasa nashangaa watu wanahofia nini, kilichobaki ni kwa mashabiki tu kuujaza uwanja ili timu ihamasike kufanya vizuri.
“Uwanja ukijaa Mzize (Clement) atafanya vizuri, mashabiki wakijazana uwanjani Fei Toto (Feisal Salum) atapambana, sasa tusisubiri hadi Ijumaa, tuanze sasa kununua tiketi mapema ili tuujaze uwanja wetu,” amesema Kamwe.
Taifa Stars imetinga robo fainali kufuatia kuongoza Kundi B kwa kukusanya pointi 10 zilizotokana na kushinda mechi tatu na sare moja, huku inakutana na Morocco iliyokamata nafasi ya pili Kundi B na pointi tisa baada ya kushinda mechi tatu na kupoteza moja.