Moshi. Zikiwa zimepita siku 47 tangu aliyekuwa Diwani wa Kiboriloni kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Frank Kagoma kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), leo Jumatatu, Agosti 18 ametangaza kurejea upinzani kwa kutimkia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Kagoma, ambaye katika baraza la madiwani lililopita Manispaa ya Moshi, alikuwa diwani pekee wa Chadema, alijiunga na CCM Julai 2, 2025 na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai.
Baada ya kujiunga na CCM, alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea udiwani Kata ya Kiboriloni, lakini alishindwa katika kura za maoni baada ya kushika nafasi ya pili kwa kura 30, wakati mgombea aliyeongoza alipata kura 119.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi ya Chaumma, Kagoma amesema ameamua kujiondoa CCM baada ya kuamua kubadilisha gia angani na kushindwa kutimiza dhamira yake ya kugombea udiwani katika kata ya Kiboriloni katika chama hicho.
“Ni kweli hivi karibuni nilijiunga na CCM nikitokea Chadema na nilijiunga huko baada ya kuniambia mimi ninawafahamu watu wa Kiboriloni na wapo tayari kuniomba kupeperusha bendera kugombea udiwani kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu,” amesema Kagoma na kuongeza kuwa.

“Lakini ghafla katikati wakaamua kubadilisha gia angani wakaniacha wami, gari ya Chaumma ikawa inapita ikanipa lifti, sasa anayekupa lifti ndiye anayekujali na ndiyo unaenda naye,” amesema.
Aidha amesema tayari amechukua fomu kuomba kuteuliwa na Chaumma kugombea udiwani katika kata ya kiboriloni na kwamba kwa sasa wanasubiri mchakato wa kura za maoni.
“Tayari nimechukua fomu kuomba ridhaa ya Chaumma kugombea udiwani kata ya Kiboriloni na sasa tuliotia nia tumekuwa watatu, tunasubiri mchakato wa kura za maoni kuona atakayeteuliwa kugombea”.
Akizungumza Katibu wa Chaumma Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amesema wameendelea kupata nguvu katika chama hicho na wana matumaini makubwa ya ushindi katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
“Leo Agosti 18, Chaumma tumempokea mwanachama wa CCM, Frank Kagoma ambaye pia alikuwa mtiania wa udiwani katika kata ya Kiboriloni kupitia chama hicho. Tayari amechukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea kupitia Chaumma, tunamtakia mema na tumeona nguvu ya umma,” amesema Lema.
Amedai: “Ni moja wapo ya shambulio kwa Chama cha Mapinduzi kutokana na kwamba walimchukua ili kudhoofisha upinzani kwa ahadi kadhaa ikiwemo za kugombea udiwani, lakini baada ya kugundua ahadi hiyo haikuwa ya kweli amelazimika kuomba kurudi nyumbani na sisi tumempokea.”
“Tumeona ni vyema kwani amerudi na watu wengi. Tuseme kwa sasa tuna nguvu na katika uchaguzi huu kama hakutafanyika figisu lazima CCM watajua tuko salama kupitia Chaumma,” amesmea.