Arajiga apewa mechi ya lawama CHAN, mbongo mwingine uhakika

Hatimaye Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemkumbuka refa Ahmed Arajiga wa Tanzania baada ya kumpanga kuchezesha mechi ya mwisho ya kundi C ya CHAN 2024 baina ya Algeria na Niger, leo Jumatatu, Agosti 19, 2025 katika Uwanja wa Nyayo, Nairobi kuanzia saa 2:00 usiku.

Kabla ya mchezo wa leo, Arajiga hakuwahi kuchezesha mechi yoyote ya fainali za CHAN 2024 zinazoendelea katika nchi za Tanzania, Uganda na Kenya yeye pamoja na Mtanzania mwenzake Hamdani Said ambaye ni refa msaidizi.

Arajiga ikumbukwe ndio mshindi mara mbili mfululizo wa tuzo ya Refa Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu ya 2023/2024 na 2024/2025.

Katika mechi ya leo, Arajiga atasaidiwa na Diana Chikotesha wa Zambia na Abdul Aziz Jawo wa Gambia huku refa wa akiba akiwa ni Tsegay Mogos wa Eritrea.

Mchezo huo wa leo ni wa uamuzi kwani Algeria inahitaji ushindi na kisha kuiombea nuksi Afrika Kusini inayocheza na Uganda ili yenyewe iweze kufuzu.

Kama Algeria itatoka sare au kupoteza, Afrika Kusini inaweza kusonga mbele ikiwa itapata ushindi dhidi ya Uganda katika mechi nyingine inayochezwa jijini Kampala leo kuanzia saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.

Uganda yenyewe inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote dhidi ya Afrika Kusini ili ijihakikishie kufuzu Robo Fainali.

Katika mechi hiyo ambayo Arajiga atakuwa refa wa Kati, Mtanzania mwingine Alfred Amede naye amepangiwa majukumu ya kuwa mmoja wa maofisa wa mchezo huo.

Amede amepangwa kuwa Ofisa Mkuu wa Udhibiti wa Dawa za Kusisimua Misuli, jukumu ambalo alianza nalo katika mechi za kundi A.