SIKU moja baada ya kutua Mlandege, kocha wa Abdallah Mohamed ‘Baresi’ amesema wana kazi kubwa ya kufanya kuipambania timu hiyo kufanya vizuri kimataifa.
Baresi amejiunga na timu hiyo akiwa kocha huru baada ya kuachana na Mashujaa inayoshiriki Ligi Kuu Bara, akizungumza na Mwanaspoti alisema anayo furaha kujiunga na timu hiyo, lakini ana kazi kubwa ya kufanya ili kuisaidia iweze kuvuka hatua inayofuata.
“Ni kweli nimepata hii nafasi ni heshima kwangu ili kuilinda ni kuhakikisha naiandaa vizuri, iweze kuwa timu shindani kimataifa hasa kutoa uteja wa kuishia hatua za awali,” amesema Baresi na kuongeza;
“Nimekaa na uongozi na benchi nililolikuta kushauriana kulingana na timu ilivyo nimeona kuna mapunguvu hivyo tujue ni namna gani tutafanya ili kuwa na kikosi imara na cha ushindani japo nimesikia kuna usajili umefanyika nasubiri kuona.”
Wakati huo huo, Baresi amefunguka sababu za kushindwana kubaki Bara baada ya kuhusishwa na Tanzania Prisons akiweka wazi walishindwana kimaslahi.
“Ni kweli nilifanya mazungumzo na Prisons sijaweza kwenda huko kutokana na kushindwana kwenye maslahi na ndipo nilipoamua kurudi nyumbani na sasa naitumikia Mlandege.
“Kufundisha ndio kazi yangu hivyo naifanya kwa maslahi naamini nimefanya uamuzi sahihi kurudi nyumbani nipo tayari kuipambania Mlandege iweze kufanya vizuri.”
Mwanaspoti limezinasa za ndani kuwa mara baada ya kumaliza majukumu ya michuano ya kimataifa Baresi atajiunga na Zimamoto inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar.