KOCHA wa Kenya, Benni McCarthy ametoa kauli inayoonekana kama ni kijembe kwa Taifa Stars ya Tanzania, huku akisisitiza wanapaswa kujipanga kikamilifu kwa mechi ya robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024 dhidi ya Morocco ambayo wao waliifunga katika makundi.
Kenya iliibuka kinara wa Kundi A lililojulikana kama ‘kundi la kifo’ ambalo pia lilihusisha Morocco na DR Congo. McCarthy alisema safari hiyo haikuwa rahisi na sasa ni zamu ya Tanzania.
“Tanzania watapata walichokuwa wakikitaka, kwa sababu sasa wanakutana na Morocco. Watajionea yale ambayo sisi tumeyapitia kila mechi kwenye kundi hili. Natarajia kusikia mrejesho baada ya mchezo huo, ili wajue tulivyopambana. Nawatakia kheri,” alisema McCarthy.
Katika mechi ambayo Kenya iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco, McCarthy alisema kutumia mbinu za kocha wake wa zamani, Jose Mourinho aliyemfundisha wakati akiichezea FC Porto ya Ureno.
Mbinu hizo ni kuziba mianya ya wapinzani hasa unapokuwa pungufu katika mechi hiyo, Kenya ilicheza muda mrefu ikiwa pungufu na mpango kazi wao ulifanya kazi vizuri baada ya Chrispine Erambo kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 45+4.
Kwa upande wao, Kenya imetinga robo fainali ikiwa na morali ya juu, McCarthy anaamini uzoefu wa kukabiliana na vigogo kama Morocco na DR Congo kwenye hatua ya makundi utawapa nguvu ya kufanya vizuri zaidi.
Kwa upande wa Taifa Stars, ujumbe wa McCarthy unaweza kutafsiriwa kama tahadhari kabla ya kuwavaa vigogo hao.