CHAN 2024: Mechi 32 mabao 66, Mmoroco akimbiza

KABLA ya mechi mbili za jana za Kundi C, rekodi zilikuwa zikionyesha jumla ya mabao 66 yametinga wavuni kupitia mechi 32, huku mshambuliaji Oussama Lamlioui akiongoza orodha ya wafungaji akiwaburuza wachezaji wa timu nyingine 18 zinazoshiriki CHAN 2024.

Michuano hiyo ya CHAN ilianza rasmi Agosti 2 na inatarajiwa kufikia tamati Agosti 30 na bingwa atafahamika, lakini hadi sasa Lamlioui anayeichezea RS Berkane amefunga mabao matatu, yakiwamo mawili aliyofunga juzi wakati Morocco ikiiondosha DR Congo kwa kisago kwa 3-1.

Ushindi wa Morocco umeifanya timu hiyo kuifuata Tanzania katika hatua ya robo fainali, mechi itakayopigwa Jumamosi Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia saa 11:00 jioni.

Nyota huyo wa Morocco anawaongoza mastaa wengine 10 akiwamo Clement Mzize wa Tanzania ambao kuila mmoja amefunga mawili na nyuma yao kuna orodha nyingine ndefu ya waliofunga bao moja moja, wakiwamo wawili waliojifunga katika fainali hizo za nane zilizoshuhudia pia penalti 10.

Mzize amefunga mabao mawili kama ilivyo kwa Austin Odhiambo na Ryan Ogam (wote wa Kenya),

Joao Manha ‘Kaporal’  (Angola), Thabiso Kutumela(Afrika Kusini), Allan Okello (Uganda), Abdelrazig Omer (Sudan), Lalaina Rafanomezantsoa (Madagascar), Japhte Kitambala(DR Congo) na Mohamed Hrimat(Morocco).

Wachezaji walijifunga (kabla ya jana) walikuwa ni; Quinito wa Angola na Leonard Ngenge (Nigeria) waliofanya watimize idadi ya mabao 66 yaliyokuwa yamefungwa kabla ya mechi za jana, huku nyota wanne wakiwa wamelimwa kadi nyekundu Kenya ikiongoza kwa kuna na kadi mbili.

Waliolimwa kadi nyekundu ni Andriamirado Dax wa Madagascar aliyekuwa mchezajui wa kwanza, kisha wakafuata Wakenya wawili, Marvin Nabwire na Chris Erambo waliopewa kupitia mechi mbili tofauti na Abdoulaye Toure wa Burkina Faso.

Hata hivyo, namba hizo zilizopo kwa sasa katika CHAN 2024 zinatarajiwa kubadilika kupitia mechi za jana na zitakazopigwa leo kufunga hesabu kwa hatua ya makundi kabla ya kupigwa mapambano ya robo fainali ambapo timu sita zimefuzu hatua hiyo.