BAADA ya makundi A na B kumaliza kazi na kutoa timu nne za kucheza hatua ya robo fainali, leo Jumatatu ni zamu ya Kundi C, huku wenyeji Uganda wakiwa na kibarua kizito mbele ya Afrika Kusini, kwani timu mojawapo ikizembea baada ya dakika 90 itaiaga michuano hiyo.
Uganda na Afrika Kusini zinatarajiwa kuvaana katika mechi ya kufungia kundi itakayopigwa kuanzia saa 2:00 usiku sambamba na pambano jingine la kundi hilo kati ya Algeria na Niger iliyoaga mapema.
Wenyeji wanaongoza msimamo kwa sasa wakiwa na pointi sita kutokana na mechi tatu kama ilizocheza wapinzani wao hao, lakini wanatofautiana alama kwani Afrika Kusini ina pointi nne kama ilizonazo Algeria inayokutana na Niger iliyovuna alama moja na kuaga fainali hizo za nane.
Ushindi au sare yoyote ndiyo utakaoihakikishia Uganda kusalia katika michuano hiyo, lakini kipigo kinaweza kuitupa nje iwapo Algeria itaifanyia kweli Niger, kwani Sauzi na Mbweha wa Atlasi hao kila moja itafikisha pointi saba na kuing’oa The Cranes na alama sita zilizonazo kwa sasa.
Hivyo, mechi za leo ni ngumu kwa kila timu hususan wenyeji iliyoandaa fainali za CHAN 2024 kwa mara ya kwanza ikishirikiana na Tanzania na Kenya, wakiwa pia ndio watakaokuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Uganda iliyoanza michuano kwa kipigo ca aibu cha mabao 3-0 kutoka kwa Algeria kabla ya kuzinduka mbele ya Guinea waliyoifumua mabao 3-0 na kuichakaza Niger kwa 2-0, itaendelea kumtegemea Allan Okello mwenye mabao mawili hadi sasa, Ivan Ahimbisibwe na Reagan Mpande, ili kupenya robo kuzifuata Tanzania na Kenya zilizotangulia sambamba na Madagascar.
Hata hivyo, itakuwa na kibarua kigumu mbele ya nyota wa Afrika Kusini wanaoongozwa na nahodha Neo Maema na wengine ambao katika mechi tatu zilizopita za kundi hilo wameonyesha uwezo mkubwa hasa wa kujilinda na kutengeneza mashambulizi makali.
Rekodi inayongeza Uganda haijawahi kutamba mbele ya Wasauzi katika mechi sita walizokutana tangu mwaka 2004 katika michuano mbalimbali ikiwamo ya kuwania fainali za Kombe la Dunia, Afcon, Cosafa na hata kirafiki, kwani imepoteza mara nne na kuambulia sare mbili tu.
Mara ya mwisho kukutana ilikuwa katika mechi za makundi kuwania fainali za Afcon 2025 ambapo Uganda ilipasuka nyumbani kwa mabao 2-0 Novemba 15, mwaka jana baada ya awali kutoka sare ya 2-2 ugenini Septemba 6, 2024.
Hata hivyo, faida ya kucheza mbele ya mashabiki wao, inaweza kuibeba Uganda katika mechi hiyo ya leo, lakini inapaswa isijiamini sana kwa aina ya soka inalocheza Afrika Kusini.
Katika mechi nyingine ya leo Algeria inahitaji ushindi mbele ya Niger inayokutana nao kwa mara ya 12 tangu mwaka 1981, huku yenyewe ikibebwa na rekodi tamu ya kushinda mara 10 dhidi ya moja ya wapinzani wao.
Mara ya mwisho zilipokutana katika mechi za makundi za kuwania fainali za Afcon 2025, Algeria ilishinda nje ndani kwa ushindi wa 2-1 na 1-0, hivyo kuonyesha huenda leo isiwe na kazi ngumu ya kukata tiketi ya kucheza robo fainali mbele ya wapinzani wao hao.
Hata hivyo, Algeria inapaswa kushuka uwanjani kwa tahadhari kubwa, kutokana na ukweli katika mechi iliyopita Niger iliiduwaza Afrika Kusini kwa kuibana na kutoka nao suluhu huku ikiupiga mwingi, lakini kama itaendelea kucheza soka lile lile la kutokata tamaa basi dakika 90 zitawabeba.