CHAN 2024: Wamorocco waingiwa ubaridi

KOCHA wa timu ya taifa ya Morocco kwa wachezaji wa ndani, Tarek Sektioui amekiri hajawa na muda wa kuangalia kwa undani mechi za Taifa Stars ambao watakabiliana nao, Jumamosi ya Agosti 22 kwenye mechi ya robo fainali mashindano ya CHAN 2024.

Morocco ambayo ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A ikiwa na pointi tisa nyuma ya Kenye, itawabidi kuja Tanzania kucheza dhidi ya kinara wa kundi B, Taifa Stars iliyoweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika mashindano hayo kutinga robo.

“Kwa kweli sijapata nafasi ya kuangalia mechi nyingi za Tanzania kwa sababu tulipokuwa hapa (Kenya), akili yangu ilikuwa  katika mechi za  kundi letu. Lakini bila shaka tunatarajia mchezo mgumu kwa sababu wao pia ni timu inayocheza katika ardhi yao ya nyumbani,” alisema kocha huyo.

Kauli hiyo ya Tarek inathibitisha namna ambavyo Morocco inaipa heshima Stars ambayo licha ya kuwa hii ni mara yake ya tatu kushiriki michuano hiyo imeonyesha kiwango bora katika hatua ya makundi.

Sektioui anajua kukutana na Tanzania si jambo rahisi, hasa ikizingatiwa nguvu ya sapoti ya mashabiki na faida ya kucheza nyumbani, hali inayoongeza presha kwa kila mpinzani anayekutana na Stars.

Morocco ambao walipoteza mechi moja tu katika hatua ya makundi dhidi ya Kenya kwa bao 1-0 ni mabingwa mara mbili wa michuano hiyo ambayo ilianzishwa miaka 15 iliyopita.