China kuja na roboti inayobeba ujauzito, wataalamu wapinga

Inawezekana ni wakati wa ajabu kuishi duniani kwa sasa, dunia ilianza kushuhudia roboti zikifanya kazi mbalimbali, migahawani, kuwa dada wa kazi na hata kuolewa, lakini sasa mambo yameenda mbali zaidi kwani wanasayansi kutoka China wapo mbioni kuleta roboti zitakazokuwa na uwezo wa kubeba mimba.

Tovuti ya New York Post, ilinukuu taarifa zilizochapishwa na tovuti ya Chosun Biz, China inafanya kazi ya kubuni roboti yenye tumbo la uzazi bandia  litakalopokea virutubisho kupitia bomba na litakuwa na uwezo wa kubeba kijusi kwa takribani miezi 10 kabla ya kujifungua.

Inaelezwa wazo la kuunda roboti mwenye uwezo wa kubeba ujauzito lilibuniwa  na Dk Zhang Qifeng, mwanzilishi wa kampuni ya Kaiwa Technology, yenye makao yake Guangzhou, China.

Taarifa pia zimefichua kwamba  ikiwa kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, muundo wa kwanza wa roboti hiyo  utazinduliwa mwaka ujao.

Kwa wale wanaopata changamoto ya kushika mimba, wataweza kumkodisha roboti huyo ili kuwabebea mimba zao kwa gharama ya takriban Yuan 100,000 (sawa na Sh36 milioni) kiasi ambacho ni kidogo zaidi ikilinganishwa na gharama ya kumkodisha mwanadamu wa kawaida ambaye kwa nchi kama Marekani inaweza kufikia Dola 100,000 (zaidi ya Sh260 milioni) gharama zote kwa ujumla.

“Teknolojia ya tumbo la uzazi bandia tayari iko katika hatua nzuri na sasa inahitaji kupandikizwa ndani ya tumbo la roboti ili mtu halisi na roboti waweze kushirikiana kufanikisha kuunda ujauzito na kuruhusu kijusi kukua ndani,”alisema Qifeng  kupitia tovuti ya Chosun Biz.

Hata hivyo, bado kuna maswali mengi hayajajibiwa kwa sasa, ikiwemo jinsi mbegu ya kiume na ya kike zitakavyounganishwa na kuingizwa tumboni, na vilevile jinsi roboti atakavyoweza kujifungua.

“Tumefanya majadiliano na mamlaka za mkoa wa Guangdong na tumewasilisha mapendekezo husika huku tukijadili sera na sheria,” alisema daktari huyo, akijibu wasiwasi wa watu ambao wameibua hoja za kwamba huenda kukawa na ukiukwaji wa sheria.

Kupitia utafiti uliofanywa na tovuti ya The Guardiana, unaeleza Baadhi ya wadau wa masuala ya afya na haki za binaadamu  wameilaani teknolojia hii  wakisema ni kumnyima kijusi uhusiano wa mama, hivyo  ni jambo lisilo la kimaadili na ni ukatili.

Gazeti la Kichina la  The Standard liliripoti kuwa baadhi ya wataalamu wa afya wana mashaka juu ya uwezo wa teknolojia hii jinsi itakavyofanya kazi katika mchakato wa kibayolojia wa ujauzito.

Wanasayansi hao walisema kuna mambo ambayo sio sawa kufanyika kupitia roboti kama vile kutolewa kwa homoni za mama.

Andrea Dworkin, mwandishi na mwanaharakati  wa haki za wanawake, aliwahi kukosoa teknolojia ya tumbo la uzazi bandia kwa hofu kuwa inaweza kusababisha kile alichokiit…mwisho wa wanawake.

Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Watoto ya Philadelphia na kuchapishwa mwaka 2022 ulionyesha hofu ya kuwapo kwa teknolojia hiyo.

Hata hivyo, wapo wanaosema kuwa matumbo ya uzazi bandia yanaweza kuwaokoa wanawake dhidi ya hatari za ujauzito, ili wasibebe tena mimba ambayo muda mwingine huja na madhara.

Imeandikwa na Mustafa Mtupa kwa msaada wa mashirika ya habari.