Fadlu ni kazi tu huko Misri

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids amesema mazoezi anayoendelea kuyatoa katika kambi iliyopo nchini Misri yatampa picha ya wachezaji atakaoendelea kusalia nao na wale ambao watapewa mkono wa kwaheri.

Fadlu ameliambia Mwanaspoti kwamba, bado hawajafunga usajili na endapo kukitokea mahitaji ya kutaka wachezaji wengine watafanya hivyo na kuachana na wale ambao hawaoni umuhimu wa kuendelea nao msimu ujao.

“Katika maandalizi ya msimu kunahitajika umakini wa hali ya juu kwa maana ya kuandaa kikosi imara. Ndiyo maana tunapata muda mwingi wa kuwaangalia (wachezaji) na kufanya nao mazoezi yatakayoleta ushindani katika michuano mbalimbali itakayokuwa mbele yetu,” alisema Fadlu na kuongeza:

“Kwa wachezaji watakaoachwa watatafutiwa utaratibu mzuri wa kuhakikisha wanapata timu za kwenda kuzitumikia, hiyo ni kazi yao lazima waendelee kupambana na nimekuwa nikiwaambia mara nyingi ili wafanikiwe lazima wajitume kwa bidii na kuzingatia nidhamu.”

Kuhusiana na wachezaji wapya waliyojiunga na timu hiyo baadhi yao wakiwa  Rushine De Reuck, Allasane Kante, Morice Abraham,  Hussein Daudi Semfuko na  Jonathan Sowah alisema wameanza kuingia katika mfumo wa kuendana na wenzao waliyokuwepo msimu uliyopita.

“Mazoezi yananipa matumaini ya mbele kutatengenezwa kitu kikubwa na kizuri ambacho kitazaa matunda baada ya kuanza majukumu yetu ya msimu ujao,” alisema Faldu.

Fadlu kwa msimu wake wa kwanza wa 2024/25 kuifundisha Simba aliisaidia kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 78 na ilifika fainali za CAF ikitoka bao 1-1 dhidi ya  RS Berkane nyumbani.