Hamad Rashid na ahadi ya kuinua kilimo Zanzibar

Pemba. Mtiania kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed amesema endapo wananchi wakimchagua ataelekeza nguvu zake kwa wakulima, kilimo chao kiwe cha tija.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Agosti 18, 2025 wakati akizungumza na wananchi na wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara wa kuwatambulisha wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo ubunge, uwakilishi na udiwani uliofanyika Gombani Kisiwani Pemba.

Amesema wakulima wamekuwa wakishindwa kulima kilimo cha kisasa kwa kukosa huduma muhimu zikiwemo pembejeo pamoja na elimu jambo linalowafanya kupata mavuno hafifu.

Amesema iwapo wananchi watamchagua kuwa kiongozi wao atawapatia vifaa vya kilimo cha umwagiliaji vitakavyochangia kuongeza  uzalishaji ili kukuza kipato chao na kuleta mabadiliko katika maisha yao.

Mbali ya kuwawezesha kwa dhana za kilimo pia atawawezesha kielimu kwani baadhi yao hawana utaaluma wa kilimo cha kisasa kitakachokuza uchumi wao.

Ameongezea endapo yote yatafanikiwa hao wakulima watazalisha mpunga utakaowawezesha kupatikana mchele kwa wingi ambapo watakula wao wenye na mwingine kuuza nje ya Zanzibar, hivyo kuachana na uagizaji mchele kutoka nje ya nchi.

 “Hekta moja ya mpunga iliyomwagiliwa maji kwa kutumia utaalamu ina uwezo wa kuzalisha tani tatu mpaka tano ni sawa na kilo 1,500 za mchele kwa hiyo hekta elfu 10,000 zilizopo Zanzibar kama wakulima 30,000 wakitengenezwa vizuri Zanzibar itajitegemea kwa chakula na itauza hata nchi nyingine,’’ amesema.

Katika hutua nyingine, Hamad amesema ataandaa programu maalumu itakayowawezesha wanafunzi kusoma kwa njia ya kidijitali badala ya kutumia karatasi.

 “Tayari katika chama chetu tuna programu maalumu tunayoiandaa kwa tunataka wanafunzi wasome kwa kutumia mifumo ya teknolojia ili kuendana mabadiliko ya teknolojia,’’amesema.

Aidha Hamad amewataka wananchi na wanachama wa chama hicho kutosikiliza maneno ya wanasiasa mbalimbali ya kuvuruga amani iliyopo, badala yake wawe mstari wa mbele katika kuhimizana kuiimarisha.

Akitoa salamu za wazee wa chama hicho, Abdi Abasi Mohammed amesema cha hicho kina sera za kisasa zinazotekelezeka kwa maendeleo ya Taifa ili kuinua hali ya ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii.