HANDENI MJI YAJA NA MWAROBAINI WA UTORO SHULENI
Na Mwandishi Wetu, Handeni
HALMASHAURI ya Mji Handeni, mkoani Tanga kupitia Idara ya Elimu Msingi imepongezwa kwa kubuni mkakati maalum unaoongeza uwajibikaji wa wazazi katika kukabiliana na utoro shuleni.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 18, 2025 mjini hapa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, Mhe. Salum Nyamwese katika kikao na Menejimenti ya Halmashauri hiyo (CMT).
Amesema mkakati huo unaongeza ushiriki wa wazazi na viongozi wa mtaa na kata katika kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wanafunzi ili kudhibiti utoro kwa shule za msingi na kwamba ubunifu huo pia utafanyika kwa shule za sekondari.
Amesisitiza watumishi wa halmashauri hiyo kuwa wabunifu katika utendaji kazi wao ili wananchi waendelee kupata huduma bora.
Pamoja na hayo, Nyamwese amehimiza uwajibikaji, ushirikiano na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea ili matokeo yaonekane kwa wananchi.
“Hakikisheni mnaweka mbele maslahi ya wananchi na taifa kwa kutoa huduma bora kwa wananchi wetu, sisi ni rasilimali ya umma kutokana na dhamana tulizopewa ni mali ya umma, wajibu wetu ni kufanya kazi kwa nidhamu,”amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Maryam Ukwaju ameishukuru serikali kwa kuongeza watumishi wapya wa kada mbalimbali ambazo awali vitengo na idara zilikuwa zikikabiliwa na upungufu wa watumishi.
Pia, ameahidi kufanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na Kiongozi huyo ikiwamo kuendelea kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa mapato.