Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikitarajia kusomewa uamuzi wa maombi yao ya kufunguliwa kifungo cha zuio la kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali zake, Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu anatarajiwa kusomewa ushahidi wa kesi ya uhaini inayomkabili.
Matukio hayo mawili yanatarajiwa kufanyika leo, Agosti 18, 2025 kutokana na kesi mbili tofauti ambazo zimekuwa zikiwakutanisha mahakamani viongozi na wanachama wa chama hicho, kufuatilia mienendo yake, katika mahakama mbili tofauti.
Wakati uamuzi wa zuio dhidi ya chama hicho kufanya siasa na kutumia mali zake unatarajiwa kutolewa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Lissu anatarajiwa kusomewa ushahidi wa kesi hiyo inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Katika mazingira hayo viongozi na wanachama hao wa Chadema ambao wamekuwa wakifuatilia mienendo ya kesi hizo watalazimika kufanya uchaguzi wa wapi waende.
Hata hivyo kwa kuwa kesi ya chama Mahakama Kuu inatarajiwa kusomwa tu uamuzi, bila shaka itamalizika mapema kuliko ya Lissu iliyopo Mahakama ya Kisutu ambayo mwenendo wake utachukua muda mrefu. Hivyo watakaoanzia Mahakama Kuu wakimaliza wanaweza kuhamia Mahakama ya Kisutu.
Lissu anakabiliwa na kesi hiyo mahakamani hapo, ilikofunguliwa kwa ajili ya maandalizi ya awali, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa upelelezi, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu itakakosikilizwa katika hatua ya ushahidi na kuamuliwa.
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, Lissu anakabiliwa na shitaka mola la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.
Anadaiwa kuwa kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Mara ya mwisho ilipotajwa, Agosti 13, 2025, Jamhuri iliieleza Mahakama kuwa tayari imeshawasilisha hati ya mashtaka Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 262 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Marejeo ya 2023.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga alieleza kuwa tayari kesi hiyo imeshasajiliwa kwa usajili wa kesi ya jinai namba 19605 ya mwaka 2025.
Vilevile Wakili Katuga aliiomba Mahakama iamuru kusitishwa kesi hiyo kurushwa mubashara hasa wakati wa kusoma maelezo ya mashahidi hao ili kutekeleza amri ya Mahakama Kuu.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Hussein Mtembwa Agosti 4, 2025 iliamuru mashahidi ambao ni raia, kutoa ushahidi bila kuonekana majina na taarifa zao zinazoweza kufanya wakatambulika, familia zao na watu wote wa karibu kutowekwa wazi, kufuatia maombi ya Jamhuri.
Hivyo Wakili Katuga alidai kuwa kuna taarifa ambazo zinaweza kufanya mashahidi hao wakajulikana kama itarushwa mubashara.
Hoja hiyo ilibua mabishano makali baada ya Lissu kuyapinga maombi hayo.
Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo mpaka leo, kwanza kwa ajili ya kutolea amri hoja hiyo ya Jamhuri kusitisha urushaji wa mwenendo huo mubashara wakati wa usomaji wa maelezo hayo ya mashahidi.
Pia Hakimu Kiswaga alizitaka pande zote kuwa tayari kwa ajili ya hatua inayofuata ya mwenendo kabidhi (committal proceedings).
Katika hatua hiyo mshtakiwa husomewa maelezo ya mashahidi wote wa upande wa mashitaka wanaotarajiwa kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo, pamoja na vielelezo vinavyotarajiwa kutumika.
Baada ya hatua zote zilizoelekezwa katika sheria katika hatua hiyo, Mahakama humtaarifu mshtakiwa kuwa sasa kesi yake imehamishiwa rasmi Mahakama Kuu ambako itasikilizwa kwa tarehe itakayopangwa baada ya taratibu za awali kukamilika.
Lissu tayari alishaiarifu Mahakama kuwa alishajiandaa kwa hatua hiyo huku akibainisha kwamba ameandaa maelezo yake kurasa 102 ambayo atayatoa wakati wa mwenendo huo kabidhi, maelezo ambayo yumkini yatakuwa ni utetezi wake anaotarajiwa kuutoa wakati atakapojitetea Mahakama Kuu, kama atapatikana na kesi ya kujibu.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Walalamikaji wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali fedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho
Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sambamba na kesi hiyo pia walalamikaji hao walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba Mahakama hiyo itoe amri ya kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo ya msingi itakapoamuliwa.
Jaji Mwanga katika uamuzi wake alioutoa Juni 10, 2025 alikubaliana na hoja za walalamikaji.
Hivyo alitoa amri ya zuio kwa walalamikiwa kujishughulisha na shughuli zozote za kisiasa na pia ikawazuia wao binafsi wakala wao, au mtu yeyote anayefanya kazi kwa maelekezo au kwa niaba yao kutumia mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Walalamikiwa hawakukubaliana na uamuzi huo, hivyo wakafungua shauri la marejeo namba 14982/2025, wakiiomba Mahakama hiyo irejee na kisha iondoe amri zake hizo wakidai kuwa zilitolewa isivyo halali, ambalo lilisikilizwa Agosti 7, 2025.
Jaji Mwanga baada ya kusikiliza pande zote alipanga kutoa uamuzi wake leo, ambao ndio utakaotoa hatima ya chama hicho kuendelea na shughuli za siasa na kutumia mali zake wakati kesi ya msingi ikiendela ua kitaendelea na kifungo hicho mpaka kesi hiyo itakakapoamuliwa.