Hii hapa ratiba kamili uchaguzi mkuu, kura ya mapema Zanzibar

Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza ratiba kamili ya uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, 2025, ambapo kura ya mapema inatarajiwa kupigwa Oktoba 28, 2025.

Akitangaza ratiba hiyo kwa waandishi wa habari leo Jumatatu, Agosti 18, 2025, Mwenyekiti wa tume hiyo, George Joseph Kazi, amevitaka vyama vya siasa vitakavyoweka wagombea pamoja na wagombea wenyewe katika ngazi mbalimbali kufuata sheria, kanuni na miongozo yote iliyotolewa na tume kuhusu uchaguzi huo.

“Hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 34(3) na (4) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, inatangaza rasmi kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025 itakuwa Jumatano ya Oktoba 29, 2025,” amesema Jaji Kazi.

“Kwa kuwa sheria ya uchaguzi imetoa nafasi ya kufanyika kwa kura ya mapema, napenda kuwajulisha kuwa upigaji wa kura ya mapema utafanyika Jumanne ya Oktoba 28, 2025, siku moja kabla ya upigaji kura ya pamoja,” amesema.

Kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha sheria hiyo, upigaji kura ya mapema utawahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi siku ya uchaguzi.

Watendaji hao ni wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wa vituo, askari polisi watakaokuwa kazini siku ya uchaguzi, wajumbe wa ZEC, watendaji wa tume na wapigakura watakaohusika na kazi ya ulinzi na usalama siku ya uchaguzi.

Ratiba kamili ya uchaguzi

Jaji Kazi amesema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa urais, uwakilishi na udiwani utaanza Agosti 28 hadi Septemba 10, saa 10:00 jioni.

Septemba 11, saa 10:00 jioni ni siku ya uteuzi wa wagombea, huku kipenga cha kampeni za uchaguzi kikitarajiwa kupulizwa siku hiyohiyo Septemba 11, saa 10:01 jioni, baada ya mgombea kuteuliwa, na kampeni hizo zikitarajiwa kuhitimishwa Oktoba 27, 2025, saa 12:00 jioni.

Kwa mujibu wa ZEC, kuhesabu na kutangaza matokeo kunatarajiwa kuwa Oktoba 29 hadi Novemba mosi.

“Tunawaomba wadau wote wa uchaguzi wakiwemo vyama vya siasa, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, asasi za kiraia, waangalizi wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla katika kipindi hiki cha uchaguzi kuendelea kudumisha amani na utulivu ili tuweze kufanikisha uchaguzi huo,” amesema.

Jaji Kazi amevitaka vyama vya siasa ambavyo vitaweka wagombea, pamoja na wagombea wenyewe katika ngazi mbalimbali, kufuata sheria, kanuni na miongozo yote iliyotolewa na Tume kuhusu uchaguzi huo.

Pia waandishi wa habari nao wametakiwa kufuata sheria katika kuandika habari za uchaguzi ambazo ni sahihi kwa wananchi ili kuwa na uchaguzi wa amani, kama ilivyo kaulimbiu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 inayosema.

Jana, Agosti 17, Kamishna Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Awadh Ali Said, aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kuacha mihemko ya kisiasa wanaposimamia uchaguzi huku tume ikiahidi kutenda haki katika uchaguzi huo.

Alikuwa akifunga mafunzo ya siku tano kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa majimbo yote 50 ya Zanzibar yaliyoanza Agosti 12, ikiwa ni safari ya kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.

Alitumia fursa hiyo pia kuwakumbusha maofisa wakati wa kutoa huduma za uchaguzi bila ya kuegemea upande wowote wa chama chochote cha siasa au kufuata maagizo ya mtu au kundi lolote la ndani au nje ya nchi.

“Nataka niwasisitize wasimamizi wasaidizi wa majimbo yote ya uchaguzi katika kutekeleza majukumu yenu mwende mkatende haki. Kila mwenye haki ya kupiga kura aitekeleze bila kikwazo na tujiepushe na mihemko ya kisiasa, kwani kufanya hivyo ni kukengeuka na kukiuka sheria na maadili ya kazi zetu,” alisema Kamishna Awadh.