Mahakama Kuu yakazia kifungo cha Chadema

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imekazia kifungo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) cha kutokufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali zake mpaka kesi inayokikabili itakapomalizika.

Mahakama hiyo imekazia kifungo hicho leo Jumatatu, Agosti 18, 2025, baada ya kutupilia mbali shauri la maombi ya marejeo lililofunguliwa na chama hicho kikiiomba Mahakama ikiondolee kifungo kwa kufuta amri zake za zuio la kufanya siasa na kutumia mali zake.

Mahakama, katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Hamidu Mwanga Juni 10, 2025, ilikizuia kwa muda chama hicho kuendelea na shughuli za kisiasa na kutumia mali zake mpaka kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali inayokikabili itakapoamuliwa.

Uamuzi huo ulitokana na maombi yaliyowasilishwa na walalamikaji katika kesi hiyo ya Kikatiba namba 8323 ya mwaka 2025 iliyofunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

‎Walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya Chadema.

‎Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‎Sambamba na kesi hiyo, pia walalamikaji hao walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa wakiiomba Mahakama itoe amri ya kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo ya msingi itakapoamuliwa.

Jaji Mwanga, katika uamuzi wake alioutoa Juni 10, 2025, alikubaliana na hoja za walalamikaji.

Hivyo alitoa amri ya zuio kwa walalamikiwa kujishughulisha na shughuli zozote za kisiasa na pia ikawazuia wao binafsi, wakala wao, au mtu yeyote anayefanya kazi kwa maelekezo au kwa niaba yao kutumia mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

‎Walalamikiwa hawakukubaliana na uamuzi huo, hivyo wakafungua shauri la marejeo namba 14982/2025 wakiiomba Mahakama irejee na kisha iondoe amri zake wakidai kuwa zilitolewa isivyo halali.

Shauri hilo lilisikilizwa Agosti 7, 2025 ambapo walitoa hoja zao, ambazo zilipingwa na jopo la mawakili wa walalamikaji Shaban Marijani, Gido Semfukwe na Alvan Fidelis.

Jaji Mwanga, katika uamuzi wake leo, ametupilia mbali shauri hilo baada ya kukataa hoja za chama hicho, uamuzi ambao unakifanya Chadema kiendelee na kifungo mpaka kesi hiyo itakapomalizika au kama itakavyoamuliwa vinginevyo na mamlaka nyingine yenye mamlaka.

Katika uamuzi huo, Jaji Mwanga ametupilia mbali sababu za Chadema kupinga amri hizo, akisema hazina mashiko kisheria kuifanya Mahakama itengue amri za awali.

Katika sababu ya kwanza, Chadema kupitia mawakili wake wakiongozwa na Dk Rugemeleza Nshala walidai kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa kutokana na maombi ya zuio hilo kusikilizwa upande mmoja baada ya wakili wao, Jebra Kambole, kujiondoa katika kesi hiyo kabla ya usikilizwaji wa maombi hayo.

Akiamua hoja hiyo, Jaji Mwanga amesema haina msingi kwa kuwa walalamikiwa hawakuitumia wenyewe haki hiyo, na kwamba halikuwa jukumu la Mahakama kuwatafuta walalamikiwa mahali walikokuwa siku hiyo.

Amefafanua kuwa awali walalamikaji waliomba shauri hilo la maombi ya zuio lisikilizwe upande mmoja, lakini akawakatalia na kuelekeza lisikilizwe pande zote. Kwa muktadha huo, wakati shauri hilo lilipopangwa kusikilizwa pande zote Juni 10, 2025, mawakili wa walalamikiwa walikuwepo na wakakubaliana na pande zote.

Hata hivyo, siku hiyo ya usikilizwaji, Juni 10, licha ya mawakili wengine wa Chadema kutokutokea, wakili Kambole alifika mahakamani na baadaye aliondoka baada ya kiapo kinzani kuondolewa kwa kukosa sifa.

Hivyo Jaji amesema kuwa kuondoka kwake haikuwa sifa nzuri kama ofisa wa Mahakama, na kwamba pia hakuieleza Mahakama siku hiyo wadaiwa kwa maana ya Mnyika na wenzake, Wadhamini wa Chadema kwanini hawakufika mahakamani.

Jaji Mwanga amesema kuwa kuwa na wakili katika kesi yako hakumuondolei mdaawa wajibu wa kufika mahakamani

“Kwa hiyo haikuwa dhambi Mahakama kuendelea kusikiliza shauri, kama ilivyoelezwa na mawakili wa wajibu maombi. Mlipewa haki ya kusikilizwa lakini wenyewe hamkuchagua kuitumia haki hiyo, hivyo hoja hiyo haina mashiko,” amesema Jaji Mwanga na kusisitiza:

“Kesi kusikilizwa upande mmoja si jambo jipya, si jukumu la Mahakama kwenda kumtafuta Mnyika alipo.”

Sababu nyingine, mawakili hao walidai kuwa Mahakama haikujiridhisha na kuzingatia vigezo vya utoaji amri ya zuio, wakifafanua kuwa lengo la amri hizo ni kudumisha hali iliyopo kabla ya mgogoro, kwani walalamikiwa walikuwa na haki ya kufanya siasa na kutumia mali za chama.

Huku akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika rufaa ya Augustine Lyatonga Mrema na wenzake dhidi ya Abdallah Majengo na wenzake ya mwaka 1999, wakili Nshala alidai kuwa Mahakama Kuu haipaswi kuzuia haki hiyo ya kisiasa.

Badala yake, alidai kuwa kama kuna jambo haliko sawa, mtu pekee anayeweza kuingilia haki hiyo ni Msajili wa Vyama vya Siasa chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa kifungu cha 46.

Hata hivyo, Jaji Mwanga amesema kuwa uamuzi wa kesi ya Mrema hauwezi kutumika katika shauri hilo kwa kuwa hoja zilizokuwa zinabishaniwa katika kesi ya Mrema ni tofauti na za shauri hilo.

Kuhusu amri ya zuio la mali, wakili Nshala alidai kuwa haitakiwi kusababisha mali kuharibika na kwamba amri zilizotolewa zinaweza kusababisha mali hizo kuharibika kwani hazina uangalizi.

‎Alidai kuwa kwa amri hizo, Wadhamini wa Chadema hawana mamlaka ya kusimamia na kutumia mali za chama kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kwani mali nyingine kama magari, zisipotumiwa zinaweza kuharibika.

Pia amedai kuwa hakuna ushahidi kuwa mali hizo zikiendelea kuwa mikononi mwa waombaji zitaharibika.

Jaji Mwanga amesema kuwa amri aliyotoa ilihusu kuzuia mali za chama kutumika kwa shughuli za chama na si kwamba alizuia Bodi ya Wadhamini wa Chadema wasizitunze au kuziangalia na kwamba suala la udhibiti na uangalizi wa mali za chama bado linaendelea kuwa la bodi hiyo.

Kuhusu malalamiko ya watu wengine kuhusika katika zuio hilo badala ya walalamikiwa pekee waliotajwa katika kesi, yaani Wadhamini na Katibu Mkuu, Jaji Mwanga amesema kuwa, kwa mujibu wa sheria, amri inayotolewa dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa taasisi inawagusa watumishi wa kawaida na mawakala.

Kwa mujibu wa Amri ya XXXVII, Kanuni ya 6 ya Kanuni za Mashauri ya Madai (CPC), amri hizo za zuio hilo zinawafaunga wadhamini, viongozi wa ngazi zote pamoja na wanachama wa kawaida.

Baada ya kuchambua hoja hizo moja baada ya nyingine, Jaji Mwanga amehitimisha uamuzi huo kwa kusema kuwa, kwa sababu hizo alizozieleza, hawezi kutengua amri alizozitoa awali kwa kuwa ni za msingi.

“Hivyo Mahakama hii inaona kuwa maombi haya hayana mashiko, hivyo ninayatupilia mbali,” amehitimisha Jaji Mwanga.

Baada ya uamuzi huo, Jaji Mwanga ameahirisha kesi hiyo mpaka Agosti 28, 2025, itakapotajwa kwa ajili ya maelekezo kuhusiana na usikilizwaji wa kesi ya msingi.