Mahakama Yapiga Marufuku Kesi ya Tundu Lissu Kurushwa Mubashara

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepiga marufuku kurushwa mubashara (live) kwa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, katika hatua ya kusomewa maelezo ya mashahidi (committal proceedings).

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga, baada ya kukubaliana na ombi la upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, uliolenga kulinda usalama na utambulisho wa mashahidi.

Hakimu Kiswaga alisema kuwa hatua hiyo haiwazuii wananchi wala mshtakiwa kusikiliza kesi hiyo, bali inalenga kuzuia kufichuliwa kwa mashahidi wa siri.

“Kuzuia kurushwa mubashara hakumzuii mshtakiwa kusikilizwa, bali kunazuia ueneaji unaoweza kuhatarisha usalama wa mashahidi,” alisema Hakimu Kiswaga.

Kwa mujibu wa amri hiyo, vyombo vya habari au watu binafsi wamekatazwa kuchapisha au kusambaza nyaraka zozote zinazoweza kufichua majina, anuani au taarifa binafsi za mashahidi, isipokuwa kwa ruhusa ya Mahakama.

Uamuzi huu unafuatia agizo la Mahakama Kuu la Agosti 4, 2025, lililotolewa na Jaji Hussein Mtembwa, lililobainisha kuwa mashahidi ambao ni raia lazima walindwe kwa kufichwa utambulisho wao, wakati wale ambao si raia watatoa ushahidi kwa utaratibu wa kawaida.

Baada ya amri hiyo kutolewa, maafisa wa Mahakama Kuu waliokuwa wakirusha mubashara kesi hiyo walilazimika kuzima kamera zao.

Lissu anakabiliwa na tuhuma za uhaini, ambapo inadaiwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, alitoa kauli zinazodaiwa kushawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania.