Mashahidi 30 wamsubiri Lissu Mahakama Kuu

Dar es Salaam. Hatimaye kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, imehamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania ambako ndiko itakakosikilizwa na kuamuliwa huku Jamhuri ikitarajia kuwaita mashahidi 30 kutoa ushahidi dhidi yake na kuwasilisha vielelezo 16.

Katika kesi hiyo Lissu, anakabiliwa na shitaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hili Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Anadaiwa kuwa kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Kesi hiyo ilikofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya maandalizi ya awali, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa upelelezi, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu itakakosikilizwa katika hatua ya ushahidi na kuamuliwa.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano na malumbano ya hoja baina yake Lissu na upande wa mashitaka, ambapo amekuwa akiushinikiza ukamilishe haraka upelelezi na ulipokamilika akawa anashinikiza ihamishiwe Mahakama Kuu haraka.

Baada ya hatua hizo kukamilika na hati ya mashtaka kusajiliwa Mahakama Kuu leo Jumatatu, Agosti 18, 2025 imehamishiwa huko rasmi, huku jalada la kesi hiyo likifungwa rasmi katika mahakama hiyo ya chini.

Mahakama ya Kisutu imehitimisha jukumu lake katika kesi hiyo ambayo imekuwa ikisikilizwa  Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga kwa mwenendo kabidhi (committal proceedings).

Viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu inayounguruma tena leo Agosti 18,2025 mahakamani hapo.

Lissu amesomewa maelezo ya mashahidi wa Jamhuri wanaotarajiwa kuitwa kutoa ushahidi na vielelezo vitakavyotumika dhidi yake na upande wa mashitaka katika ushahidi wake.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga ameieleza mahakama hiyo kuwa Jamhuri inatarajia kuwaita jumla ya mashahidi 30 na kuwasilisha vielelezo 9.

Ilichukua takribani saa 4: 07 kwa upande wa mashitaka kumaliza hatua ya kumsomea maelezo ya mashahidi na vielelezo hivyo, kuanzia saa 5:18 asubuhi mpaka saa 9:25 Alasiri.

Baada ya upande wa mashitaka kukamilisha hatua hiyo, Lissu amepewa nafasi ya kueleza jambo lolote kabla ya Mahakama kuamuru kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu.

Lissu ametumia nafasi hiyo kuwasilisha maelezo yake aliyokuwa ameyaandika. Awali aliwahi kuitaarifu Mahakama hiyo kuwa ameandaa maelezo yake kurasa 102 ambayo kwa ajili kuyawasilisha katika hatua hiyo, lakini alipoulizwa na Hakimu Kiswaga amesema kuwa maelezo yake hayo yalikuwa ni kurasa 140.

Ameanza kuwasilisha maelezo yake hayo ambayo kimsingi yanajenga utetezi wake ambao anapaswa kuutoa Mahakama Kuu kesi hiyo itakaposikilizwa, iwapo atapatikana na kesi ya kujibu; kuanzia saa 9:28 alasiri mpaka saa 11:47 jioni.

Hata hivyo hakuweza kumaliza kuyawasilisha yote baada ya Hakimu Kiswaga kumta aishie hapo akimweleza kuwa maelezo hayo atayatoa Mahakama Kuu.

Wakati anaendelea kuwasilisha maelezo yake hayo, Hakimu Kiswaga amemuuliza kuwa yalikuwa na ukubwa gani ndio akasema kuwa ni kurasa 140 lakini mpaka wakati huo alikuwa amefikia ukurasa wa 70.

Hivyo,  Hakimu Kiswaga amemuongeza muda kidogo kisha akamtaka aishie hapo akimwambia kuwa hayo mengine atayatoa Mahakama Kuu.

Askari Magereza wakiimarisha ulinzi nje ya viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amefikishwa mahakamani hapo leo Agosti 18, 2025 kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) vya kesi ya uhaini inayomkabili

Ingawa hakutaja idadi ya mashahidi ambao anatarajia kuwaita, lakini alianza kuwataja majina, lakini Hakimu Kiswaga kamueleza kuwa hao mashahidi wake atawataja Mahakama Kuu.

Baada ya kukamilisha hatua hizo, Hakimu Kiswaga ametanga rasmi kufunga jalada la kesi hiyo mahakamani hapo na kuamuru kuwa sasa imeshahamishiwa Mahakama Kuu.

Kwa hiyo mshtakiwa huyo amerejeshwa mahabusu kusubiri hati ya wito wa kufika Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (preliminary hearing –PH) kwa tarehe ambayo itapangwa.

Katika hatua hiyo mshtakiwa husomewa muhtasari wa kesi, taarifa zinazojenga shitaka lake kisha atatakiwa kubainisha mambo anayokubaliana nayo na yale asiyokubaliana nayo, ambayo yatasainiwa na pande zote.

Baada ya hatua hiyo ndipo sasa atapangiwa tarehe ya kuanza usikilizwaji rasmi wa kesi hiyo ambapo Jamhuri itaanza kutoa ushahidi wake hasa ikijikita katika mambo yanayobishaniwa, katika kuthibitisha tuhuma anazokabiliwa nazo.

Wakati wote wa mwenendo huo leo mahakamani kama ilivyokuwa kawaida ulinzi ulikuwa umeimarishwa kila kona kuanzia nje ya geti la mahakama  hivyo, ndani ya viunga vya mahakama mpaka katika ukumbi wa mahakama.

Ndani ya mahakama ya wazi namba moja ambapo kesi ya Lissu iliitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya ushahidi na vielelezo, askari Magereza 12 wakiwemo waliovalia mzula ( ninja) kwa kufunika sehemu ya usoni walisimama ndani ya mahakama hiyo.

Kati ya hao 12, wanane walikuwa wamesimama nje ya kizimba alichokuwa amekaa Lissu huku wanne wakijipamba pembezoni mwa mahakama hiyo.

Lissu alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na kusomewa kesi ya uhaini. Tangu siku hiyo mpaka leo amefikisha siku ,131 akiwa rumande kwa kwa kuwa shitaka la uhaini linalomkabili halina dhamana.