Morogoro. Askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo) kundi la 64/2025 wametakiwa kuchukia na kupinga vitendo vyote vyenye dalili za kuhatarisha amani ya Taifa, huku wakiwa mstari wa mbele kuhubiri mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza leo Agosti 18, 2025 kwenye hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo yaliyoshirikisha wahitimu 89, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema vijana hao wanapaswa kuonyesha uzalendo wa hali ya juu, ukomavu na utayari wa kulitumikia Taifa kwa kulinda amani.
DC Kilakala amesema kuna changamoto pia za kampuni za ulinzi kutolipa mishahara kwa wakati au kulipa viwango vya chini zimeelezwa kudhoofisha ari ya vijana hao licha ya kazi ya ulinzi kutokuwa lelemama na kuhitaji heshima kubwa.
“Niwaombe kwa weledi mlionao, muwe walinzi wa amani mchana na usiku. Amani ikibomoka inachukua muda mrefu kuirudisha, hivyo lazima muwe mfano bora kwa jamii,” amesema Kilakala.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Joel Fyumagwa amesema mafunzo hayo yalihitimishwa kwa maonyesho ya ufunguaji na ufungaji silaha nyakati za mchana na usiku pamoja na ukaguzi wa gwaride.
Aidha, Fyumagwa alitaja washindi walioibuka katika nyanja mbalimbali akiwemo ni Abuu Chalamila (18) mshindi wa kulenga shabaha, Neema Mfuluki (18) mshindi wa porini, Alex Lawi (37) mshindi wa nidhamu, Raphael Mtwange (18) mshindi wa kwata na mshindi wa jumla James Rwegayula (27).

Akisoma risala ya wahitimu, Rwegayula amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo katika nyanja mbalimbali ikiwemo mbinu za kivita, usalama wa raia, huduma ya kwanza, kuzima moto, uhamiaji, sheria za Jeshi la Akiba na kupambana na rushwa.
“Tunashukuru Serikali kwa kuratibu mafunzo haya ambayo yametufundisha stadi muhimu za kijeshi na kiraia. Tunaahidi kuyatumia kulinda Taifa letu,” amesema.

Ofisa Mteule Daraja la Pili JWTZ, Vitalis Kimbe, amesema mafunzo hayo yaliyoanza Aprili 28, 2025, yalihusisha jumla ya wanafunzi 100 wakiwemo wanaume 64 na wanawake 24, lakini 11 walishindwa kuendelea kutokana na sababu za ugonjwa, utoro na utovu wa nidhamu.
Alitoa rai kwa Serikali, taasisi na kampuni binafsi kuwapa kipaumbele vijana waliopitia mafunzo hayo katika nafasi za ajira.