KATIKA kuhakikisha inakuwa na timu ya ushindani kimataifa, mabosi wao Mlandege wamemshusha mshambuliaji, Ishmael Robino kutoka Ghana.
Robino amejiunga na timu hiyo akiwa mchezaji huru na tayari ameungana na wenzake katika kambi ya mazoezi ya kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Mlandege, Hassan Ramadhan Hamis alisema mshambuliaji huyo ni sehemu ya wachezaji sita wa kigeni waliowasajili dirisha hili.
“Amewasili nchini jana jioni na leo ameudhuria mazoezi, ni mapema sana kumzungumzia ila naamini atakuwa sehemu ya mafanikio yetu kimataifa tunaimani kuwa atatusaidia,” amesema kocha huyo na kuongeza;
“Kuna wachezaji wengine wataingia leo kuhusu usajili kimataifa hatuna shaka tayari tumekamilisha kinachofanyika sasa ni kushughulikia paspoti kwa baadhi ya wachezaji ambao hawana.”
Amesema taratibu zinaenda vizuri matarajio yao ni makubwa kwa mashindano hayo ya CAF waliyorejea baada ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu uliopita.
Kocha Hamis amesema anaamini wachezaji wote wataibeba katika.michuano hiyo aliokiri ni migumu na yenye ushindani mkali.
Mlandege imepangwa kuvaana na Insurance ya Ethiopia kati ya Septemba 19 na 26 ikiwa raundi ya kwanza.