BEKI wa Mersin inayoshiriki Ligi ya Walemavu Uturuki, Mudrick Mohamed amesema malengo makubwa ya timu hiyo msimu huu ni kunyakua ubingwa utakaowawezesha kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Nyota huyo alicheza ligi ya Uturuki baada ya timu hiyo kumtazama katika mashindano ya Kombe la Dunia yaliyofanyika nchini humo na kufanya vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mudrick alisema timu hiyo imefanya usajili wa maana na kuongeza vitu muhimu ambavyo wanaamini wakipambana watakamilisha malengo ya kuwa bingwa.
Mbali na malengo ya timu, Mudrick alisema maandalizi yakikamilika mapema anaamini kuonyesha kiwango bora zaidi ya msimu uliopita.
“Msimu uliopita nilichelewa kujiunga na timu, nilikuta tayari wamecheza mechi tano, naamini huu msimu kama mambo yatakamilika mapema, basi naweza kufanya vizuri zaidi,” alisema Mudrick ambaye kwa sasa yuko nchini kwa mapumziko.
“Ligi ya Walemavu Uturuki ipo kwenye viwango vikubwa hivyo bingwa wa nchi anawakilisha na kuungana na nchi mbalimbali kucheza michuano hiyo mikubwa Ulaya.”
Huu ni msimu wa tatu kwa beki huyo kama ilivyo kwa nyota wengine wa Kitanzania, Ramadhan Chomelo anayekipiga Konya Amputee na Shedrack Hebron wa Sisli Yeditepe.