Mvua yasababisha nyumba 10 kuzingirwa na maji Musoma

Musoma. Zaidi ya nyumba 10 pamoja na kituo kimoja cha afya zimezingirwa na maji kufuatia mvua zilizonyesha katika manispaa ya Musoma usiku wa kuamkia leo Agosti 18, 2025 na kusababisha mafuriko katika baadhi ya mitaa.

Kufuatia hali hiyo, kituo hicho kilichopo Kata ya Bweri kinachomilikiwa na Kanisa la African Inland Church (ACT) kimelazimika kusitisha huduma kwa muda baada ya maji kuingia ndani.

Tayari uongozi wa kituo hicho umeanza mchakato wa kurejesha huduma ambapo hivi sasa shughuli ya usafi inaendelea ili kuruhusu matibabu kuendelea kama kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema hakuna madhara kwa binadamu yaliyojitokeza hadi sasa na tathmini inafanyika ili kujua hasara iliyotokana na hali hiyo.

“Kwa harakaharaka, chanzo cha maji haya kutuama ni kuwepo kwa baadhi ya watu waliojenga kwenye mkondo wa maji, lakini tunaendelea na tathmini, taarifa kamili itatolewa baadaye,” amesema Chikoka

Baadhi ya nyumba zilizopo katika mtaa wa Kariakoo mjini Musoma zikiwa zimezungirwa na maji baada ya mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia leo, Agosti 18, 2025.

Amesema hadi sasa kata nne zimebainika kuathirika zaidi huku kata mbili kati ya hizo zikipata madhara zaidi.

Amezitaja kata hizo kuwa ni pamoja na Bweri na Rwamlimi ambazo zimeathirika zaidi pamoja na kata za Nyakato na Kwangwa zilizopata madhara kiasi.

Chikoka ameongeza kuwa tayari amewaagiza watendaji wa kata na mitaa yote katika manispaa hiyo ya Musoma kusimamia suala zima la usafi hasa kwenye mitaro, baada ya kubainika kuwa wapo baadhi ya watu wameanzisha tabia ya kutupa uchafu mitaroni.

“Mbali na ujenzi kwenye mikondo ya maji lakini pia kuna changamoto ya mitaro kushindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa kwani kuna watu wameanzisha tabia ya kutupa uchafu mitaroni, hivyo maji yakifika badala ya kupita kwenye mitaro yanalazimika kupita juu na kusambaa kwenye makazi ya watu,” amesema.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agustino Magere amesema jeshi hilo limefanikiwa kuwaondoa watu waliokuwa wamezingirwa na maji na hakuna vifo wala majeruhi.

“Kuna watu wanne walipata mshtuko na kupelekwa hospitalini wanaendelea vizuri na wametibiwa na kuruhusiwa, taarifa zaidi tutatoa baada ya tathmini,” amesema Magere.

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Kariakoo ambao umeathirika zaidi wamesema hiyo siyo mara ya kwanza kutokea kwa mafuriko katika maeneo hayo, huku wakidai ujenzi holela ni moja ya sababu ya kuwepo kwa hali hiyo.

“Watu wanajenga ovyo, hakuna hatua zinachukuliwa dhidi yao, hii ni hatari sana, tunaomba watu wa mipango miji watimize wajibu wao, huu ujenzi holela unatakiwa kukomeshwa,” amesema Jumanne Zedi.

Kwa upande wake, Amina Sadiki amesema mvua hiyo iliyoambatana na radi ilinyesha kuanzia saa 9 usiku na kusababisha nyumba anayoishi kuzingirwa na maji kwa saa kadhaa kabla ya kuokolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Kwa sasa maji yamepungua na tunafanya usafi ili kurejea kwenye nyumba yetu ingawa vitu vyote vya ndani vimeharibika,” amesema.

Hata hivyo, amesema bado wana wasiwasi na hali itakavyokuwa kwani mvua hizo zilizoanza kunyesha usiku bado zinaendelea kidogokidogo na wana hofu kuwa huenda mvua zikaongezeka zaidi hasa wakati wa usiku.