Omary wa Fountain Gate kukaa nje wiki mbili

KIUNGO mshambuliaji wa Fountain Gate, Hashim Omary amejikuta akianza maandalizi ya msimu ujao kwa kupata jeraha la bega akiwa katika kambi ambayo timu hiyo imepiga mkoani Morogoro.

Omary ameliambia Mwanaspoti kuhusiana na jeraha hilo alilolipata akiwa katika mazoezi na daktari akamwambia atatakiwa kukaa nje kwa takriban wiki mbili ili kujiuguza kisha ataambiwa kipi cha kufanya.

“Kwa sasa nipo nyumbani nimefunga bega na plasta kulingana na maelekezo ya daktari. Baada ya wiki mbili nitakwenda kupima tena ndipo nitaambiwa kipi nikifanye,” alisema mchezaji huyo na kuongeza:

“Mwanzoni nilianza vizuri tu ikatokea siku nikaruka vibaya nikajikuta nakumbana na changamoto hiyo. Kikubwa nazingatia maelekezo ya daktari, hivyo naamini nitakaa sawa na kurejea kazini.”

Mbali na kuumia bega, msimu uliopita Omary hakucheza mechi nyingi – akicheza 10 na kufunga bao moja dhidi ya Azam FC na asisti moja aliyoitoa dhidi ya KMC, hivyo kitendo cha kuumia hatamani kififishe ndoto yake ya kufanya makubwa katika Ligi Kuu 2025/26.

“Mpira wa miguu ni ajira na sikumaliza shule kutokana na changamoto za hapa na pale za kifamilia, na nguvu zangu nimeziweka hapo ili maisha yangu yaweze kwenda mbele,” alisema Omary.

Kati ya mechi za msimu uliopita ambazo zilimfanya azungumziwe ni dhidi ya Simba baada ya kuchaguliwa na wenzake kuziba pengo la aliyekuwa kipa wa timu hiyo, John Noble, aliyetolewa kwa kadi nyekundu na mchezo kumalizika kwa kufungana bao 1-1 katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.