Polisi wamsaka mganga anayedaiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi

Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, limesema linaendelea kumsaka mganga wa kienyeji anayedaiwa kutoa ramli chonganishi iliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Qash iliyopo wilayani Babati, mkoani Manyara, Yohana Konki (17).

Yohana alifariki dunia baada ya kupigwa na wanafunzi wenzake kwa madai ya wizi wa kishkwambi, alfajiri ya Agosti 16,2025 shuleni hapo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 18, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ikiwemo kumsaka mganga huyo anayedaiwa kukimbia na familia yake baada ya tukio hilo kutokea.

“Mganga alikimbia na familia yake na baadhi ya mizigo siku ileile baada ya kusikia ramli yake imeleta shida, tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili ikiwemo kumtafuta na tunaamini tutampata,” amesema Kamanda huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Makarani, hadi sasa Jeshi hilo linawashikilia wanafunzi 11 wa shule hiyo wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo na kuwa uchunguzi unaendelea.

“Awali tuliwakamata wanafunzi 13 ila wawili tumewaondoa wamebaki 11, kati ya hao wawili mmoja ushahidi unaonyesha hakuwepo kabisa shuleni siku ya tukio,” amesema kamanda na kuongeza kuwa;

“Huyo mwingine wa pili tumemuondoa maana hata ushahidi wa wanafunzi wenzake unaonyesha kuwa yeye alikuwa anapita na pikipiki yake, ndipo akakuta tukio hilo na pikipiki yake ndiyo ilitumika kumbeba Yohana kumpeleka hospitali, tunaangalia kwenye suala hili tutamuweka wapi, ila siyo mtuhumiwa kwa sasa.”

Kamanda Makarani amedai kuwa chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo ni baadhi ya wenzake kumpiga kwa kumtuhumu ameiba kishkwambi baada ya mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo, kupoteza simu hiyo (kishkwambi), alikwenda na mwenzake kwa mganga wa kienyeji na kupiga ramli ili kumbaini mwizi.

“Walipotoka walimfuata huyo mwanafunzi na kumtuhumu wizi kisha wakamlazimisha awarudishie, alipokataa kuwa hakuiba, walimpiga na kusababisha kifo chake,” amedai kamanda huyo wa polisi.

Hata hivyo, ametoa wito kwa uongozi wa shule hiyo kufunga kamera ili kuepuka matukio kama hayo. Amesema huenda wanafunzi hao wangeweza kumbaini mwizi kuliko kutegemea ramli chonganishi.

“Tunalaani mno hilo tukio, ila kungekuwa na CCTV kamera, hapo ingeweza kuwasaidia wanafunzi kumbaini mwizi wao kuliko kwenda kupiga ramli chonganishi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Shangazi wa marehemu (Yohana), Elizabeth Konki ameeleza kusikitishwa na tukio hilo huku akisema wamekatisha ndoto za kijana wake ambaye ameuawa kifo asichostahili.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Hassan Juma amedai kuwa wanafunzi hao walimpiga mwenzao kwa kumshambulia kwa fimbo sehemu mbalimbali kutokana na majibu ya mganga wa kienyeji.

“Walipotoka kwa huyo ustadhi na kupewa majibu kuwa Konki ndiye amechukua hiyo simu, walimuuliza na alipokataa kuwa hakuchukua wakaanza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili,” amedai mwanafunzi huyo.