RC Mboni atoa utaratibu ndugu wanaosubiri waliofukiwa mgodini

Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema Serikali itawagharamia ndugu na jamaa watakaoweka kambi mgodi wa madini wa Chapakazi kunapofanyika uokozi.

Agosti 11, 2025, wafanyakazi na mafundi zaidi ya 22 wa mgodi huo walifukiwa kwenye mashimo baada ya kutitia wakati wakifanya ukarabati wa mduara wa mgodi huo.

Hadi sasa, watu saba wametolewa, kati yao wanne wakiwa wamefariki dunia na watatu wakiwa hai. Juhudi za kuendelea kuwatoa wengine 18 zinaendelea huku ndugu, jamaa na marafiki wakiwa eneo hilo wakiwasubiri wapendwa wao.

Leo Jumatatu, Agosti 18, 2025, Mboni akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio lililopo Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge amesema Serikali itawaandalia wawakilishi wa ndugu hao waliopo chini eneo maalumu.

“Tusingependa kuona watu wakipata changamoto za mahitaji wakati tayari wana huzuni, hivyo familia za watu 18 ambao bado hawajapatikana tumezishauri kuchagua wawakilishi wawili au watatu ambao Serikali itawapa mahitaji muhimu kwa muda watakaokuwa wakiwasubiri ndugu zao waliofukiwa katika ajali, bahati nzuri wamekubaliana na tayari wameshachagua wawakilishi,” amesema Mhita.

Joseph Buzuka anayesubiri mpendwa wake amesema: “Nina vijana wangu wawili wako ardhini leo ni siku ya nane tangu tukio hili litokee, tunasubiri hatima ya ndugu zetu kwa wakati huu tumejiandaa kiakili kwa namna yoyote tu wawatoe.”

Kwa upande wake, Monica Andrea amesema: “Nina kaka zangu wanne hadi sasa bado hakuna hata mmoja ambaye ametolewa, tumaini la kuwaona wakiwa hai limepotea, lakini nitabaki hapa hadi nitakapowaona hata kama ni miili yao.”