Unguja. Miradi ya maendeleo, kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, kuchangia asilimia 10 za kuwawezesha wajasiriamali, ongezeko la mapato na kutekeleza miradi ni miongoni mwa sababu za kupandishwa hadhi ya Baraza la Mji Kati na Halmashauri ya Wilaya Kusini kuwa Manispaa na Baraza la Mji.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Agosti 18,2025 katika hafla ya kukabidhi hati ya kupandishwa hadhi kwa baraza la Mji Kati na Halmashauri ya Wilaya ya Kusini.
Akitaja sababu nyingine Mkurugenzi wa Baraza la Mji Wilaya ya Kati, Dk Mwanaisha Ally Said amesema ni kutokana ukuaji wa mji na kuongezeka kwa huduma za kijamii.
“Miradi ya Maendeleo, kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, kuchangia asilimia 10 za kuwawezesha wajasiriamali, ongezeko la mapato na kutekeleza miradi 16 kabla ya kupandishwa hadhi hiyo, haya ndio yamesababisha,” amesema Dk Mwanaisha.
Hivyo, Mkurugenzi huyo amesema kupandishwa kwa hadhi kutasaidia kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kusimamia rasilimali zao vizuri.
Ameeleza kuwa, hiyo ni hatua muhimu ya kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii na miradi mikubwa ya hoteli kuwafikia kwa urahisi.
Amesema, baada ya baraza hilo kuwa Manispaa lengo ni kuboresha huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa vizimba vya taka, kujenga madakhalia (hosteli) ya wanafunzi wa vyuo vikuu, mradi wa vituo vya daladala na kujenga kiwanda cha kuchakata taka kitakachotofautisha taka ngumu na nyepesi ili mji kuwa safi.
Pia, amesema Manispaa hiyo inalenga kuboresha elimu kwa wafanyakazi juu ya ukusanyaji mapato na utunzaji wa mazingira.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Unguja, Mussa Haji Mussa amesema sababu ya kupandishwa hadhi Halmashauri hiyo ni ongezeko la miradi mikubwa, shughuli za kibiashara na miundombinu ya huduma za kijamii ikiwemo barabara, elimu, michezo na afya.
Amesema, kufikishiwa kwa huduma hizo imerahisisha ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Wilaya hiyo na hivyo wana kila sababu ya kuwa Baraza la Mji Kusini.
Mbali na hilo, amesema Halmashauri hiyo imechangia Sh250 millioni kwa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea) ili kupatiwa wajasiriamali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalumu za SMZ, Issa Mahfoudh Haji ameitaka Manispaa na Baraza hilo kuendeleza usafi kwani bado mji huo haupo vizuri.
Pia, ametoa wito kwa watendaji hao kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuendana na hadhi iliyopewa.
Naye, Waziri wa wizara hiyo, Massoud Ali Mohamed amesema jambo hilo lipo kwa mujibu wa sheria namba saba ya mwaka 2014, pia ni kielelezo cha kukua kwa uchumi katika maeneo hayo.
Hata hivyo, ametoa wito kwa watendaji hao kuwa na mipango mizuri ili kutoa matokeo chanya yenye kukidhi vigezo vya utoaji huduma nzuri.