Sababu mahakama kuzuia matangazo ‘live’ kesi ya Lissu‎

‎Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu imeamuru maelezo ya mashahidi wa Jamhuri wanaotarajiwa kutoa ushahidi wao kwenye kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kusomwa huku ikirushwa mubashara kama ambavyo kesi hiyo imekuwa ikifanyika.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mfawidhi, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga imetoa amri hiyo leo Jumatatu, Agosti 18, 2025, anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hii ya awali, kufuatia maombi ya Jamhuri.

Uamuzi huo unalenga kutekeleza uamuzi wa Mahakama Kuu wa  kuwalinda baadhi ya mashahidi wa Jamhuri katika kesi hiyo, ambao ni raia (wasio askari), kwa maana ya kutokuwekwa wazi, wala kutajwa majina yao na taarifa zao nyingine zinazoweza kufanya wakatambulika.

Lissu anakabiliwa na kesi hiyo mahakamani hapo iliyofunguliwa kwa ajili ya maandalizi ya awali, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa upelelezi, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu itakakosikilizwa katika hatua ya ushahidi na kuamuliwa.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hili Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Anadaiwa kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Mwenendo wa kesi hiyo umekuwa ukirushwa moja kwa moja (mubashara) na Kitengo cha Habari cha Mahakama ya Tanzania katika chaneli ya mtandao wa Youtube na vyombo vingine mbalimbali vya habari vya mtandaoni.

Hata hivyo, ilipotajwa Agosti 13, 2025, Jamhuri iliiomba Mahakama iamuru kusitishwa kesi hiyo kurushwa mubashara hasa wakati wa kusoma maelezo ya mashahidi hao, ili kutekeleza uamuzi wa Mahakama Kuu uliotokana na maombi ya Jamhuri.

Askari Magereza wakiimarisha ulinzi nje ya viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amefikishwa mahakamani hapo leo Agosti 18, 2025 kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) vya kesi ya uhaini inayomkabili.

Katika maombi hayo Jamhuri iliomba mashahidi hao walindwe kwa maana kutoa ushahidi wao bila kuonekana, na majina yao pamoja na taarifa zao nyingine zinazoweza kufanya wakatambulika wao au familia zao na watu wa wengine karibu yao zisiwekwe hadharani.

Jamhuri katika maombi hayo ilidai kuwa wamekuwa wakitishiwa na watu wa karibu na mshtakiwa ili wasitoe ushahidi, shauri ambalo lilisikilizwa upande mmoja.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake ulitolewa na Jaji Hussein Mtembwa Agosti 4, 2025, ilikubaliana na hoja za maombi ya Jamhuri.

Pamoja na amri nyinginezo, Mahakama Kuu iliamuru mashahidi hao watoe ushahidi wao kwa kificho (bila kuonekana mahakamani), majina yao, anuani zao, makazi yao na taarifa zao nyingine zinazoweza kufanya wakatambulika wao wenyewe, familia zao marafiki na watu wao wa karibu zisiwekwe wazi.

Amri hiyo inazuia kuchapishwa (pulication) kwa taarifa hizo wakati mwenendo kabidhi (committal proceedings) na wakati wa usikilizwaji kamili wa kesi hiyo Mahakama Kuu, isipokuwa kwa ruhusa ya mahakama hiyo.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu inayounguruma tena leo Agosti 18,2025 mahakamani hapo.

Hivyo siku hiyo kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga alieleza kurushwa mubashara kwa mwenendo huo kutakuwa ni ukiukwaji wa amri ya Mahakama Kuu.

Hoja hiyo iliibua mabishano makali baada ya Lissu kuyapinga maombi hayo, pamoja na mambo mengine akidai kuwa hakuna sababu za msingi bali Jamhuri inalenga kuleta utaratibu wakuendesha kesi hiyo gizani kwa kuwa inafuatiliwa na watu wengi.

Hata hivyo, Hakimu Kiswaga amekubaliana na hoja za Serikali na ameamuru wakati maelezo ya mashahidi hao yakisomwa yasirushwe mubashara.

Hakimu Kiswaga amesema sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai inaelekeza mwenendo wa mashauri ya jinai ya uchunguzi a awali (PI) kufanyika hadharani katika mahakama ya wazi isipokuwa vigezo vinavyohitajika ili kulinda masilahi mengine.

Pia amesema sheria hiyo inaelekeza maelezo ya mashahidi yatasomwa kwa mshtakiwa na si kwa mtu mwingine na kifungu hicho hakielezi kuhusiana na kuchapisha maelezo, sheria hiyohiyo inaeleza maagizo ya Mahakama Kuu kuhusu ulinzi yanapaswa kuzingatiwa.

Hakimu Kiswaga amesema Mahakama inatambua umuhimu wa kanuni ya uwazi na umma kusikiliza mashauri, hivyo Mahakama haitafunga mwenendo kabidhi kufanyika faragha bali kwa katika mahakama ya wazi (open court).

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu inayounguruma tena leo Agosti 18,2025 mahakamani hapo.

Hata hivyo, licha ya umuhimu huo wa uwazi, Hakimu Kiswaga amesema kuwa pia Mahakama ina jukumu la kulinda usalama wa mashahidi, faragha zao, usalama wa watoto wao au familia na masilahi mengine.

Amesema uchapishwaji na urushwaji wa mwenendo huo mubashara hupanua wigo wa maudhui kuifikia hadhira kubwa na kunaweza kusababisha taarifa za mashahidi ambao zimekatazwa na Mahakama Kuu kusambazwa, zikatambulika.

“Live stream (matangazo ya moja kwa moja mitandaoni) hutoa maudhui kwa watu wengi mara moja wakiwemo wanaoweza kumtafuta kumfichua shahidi,” amesema Hakimu Kiswaga.

Amesisitiza Mahakama inapaswa kuzingatia haki ya mshtakiwa kusikilizwa wazi na mashahidi kulindwa, huku akifafanua kuwa hatua hiyo ya usikilizwaji wa wazi ni kwa umma kuhudhuria mahakamani na si kwa njia za urushaji matangazo ya mwenendo mubashara.

“Kuzuia livestream hakumzuii mshtakiwa kusikilizwa kwa haki bali kunazuia uendeshaji wa taarifa unaoweza kuharibu ulinzi wa mashahidi na Mahakama imesema uendeshaji wa nyaraka na maelezo ya ushahidi yenye utambulisho hawezi kufanyika bila ruhusa ya Mahakama,” amesema Hakimu Kiswaga.

Amesema ili kurushwa moja kwa moja au kuchapishwa kwa mwenendo huo maombi yanapaswa kupelekwa mahakamani na Mahakama isikilize pande zote husika katika kesi na itoe kibali, kama ambavyo Mahakama Kuu ilivyoelekeza.

Viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu inayounguruma tena leo Agosti 18,2025 mahakamani hapo.

Hakimu Kiswaga amesisitiza mwenendo huo utaendelea katika mahakama lakini utangazwaji na usambazwaji wake moja kwa moja mitandaoni au uenezwaji wake kwa njia nyingine kama vipande vya picha jongefu (video clips) unazuiliwa, mpaka kwa kibali cha Mahakama hiyo au Mahakama Kuu.

Hakimu Kiswaga amesisitiza kuchapisha au kunakili nyaraka za ushahidi na taarifa za ushahidi kunakoweza kufichua anuani au taarifa nyingine zinazoweza kufichua utambulisho wa shahidi raia, unakataza na kwamba mtu au chombo chochote cha kitakachokiuka amri hiyo ya Mahakama kitachukuliwa hatua za kisheria.

“Amri hii ya kutoonyesha moja kwa moja mwenendo huu ni ya lazima na yenye uwiano ili kuzingatia maagizo ya Mahakama Kuu na kuhifadhi haki ya mshtakiwa kusikilizwa kwa uwazi katika mahakama ya wazi,” amesema Hakimu Kiswaga na kuhitimisha:

“Lakini committal proceedings, Mahakama inaamua isiende moja kwa moja kwa kuwa haki ya mashahidi kulindwa haitalindwa kama ilivyoamuriwa na Mahakama Kuu.”

Kesi hiyo imepangwa leo kwa ajili ya mwenendo kabidhi baada ya upelelezi kukamilika na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwasilisha hati ya mashitaka Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 262 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Marejeo ya 2023.

Kesi hiyo tayari imeshasajiliwa Mahakama Kuu kwa usajili wa kesi ya jinai namba 19605 ya mwaka 2025.

Hivyo baada ya uamuzi huo, Hakimu Kiswaga ameelekeza hatua ya mwenendo kabidhi iendelee, kwa mshtakiwa kwanza kusomewa hati ya mashtaka iliyosajiliwa Mahakama Kuu.

Kisha sasa anasomewa maelezo ya mashahidi wote wa upande wa mashtaka wanaotarajiwa kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo, pamoja na vielelezo vinavyotarajiwa kutumika.

Hata hivyo, Lissu tayari alishaiarifu mahakama kuwa amejiandaa kwa hatua hiyo huku akibainisha kuwa ameandaa maelezo yake ya kurasa 102 ambayo atayatoa wakati wa mwenendo huo kabidhi, ambayo ni utetezi wake anaotarajiwa kuutoa wakati atakapojitetea Mahakama Kuu, kama atapatikana na kesi ya kujibu.

Baada ya hatua zote zilizoelekezwa katika sheria katika hatua hiyo, Mahakama humtaarifu mshtakiwa kuwa sasa kesi yake imehamishiwa rasmi Mahakama Kuu ambako itasikilizwa kwa tarehe itakayopangwa.