SEKTA YA BIMA YAKUA MARA DUFU CHINI YA RAIS SAMIA



 :::::::::

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SEKTA ya bima nchini imepiga hatua kubwa ya maendeleo ndani ya miaka minne tu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku thamani ya mitaji ikiripotiwa kuongezeka kwa zaidi ya mara mbili.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), thamani ya mitaji katika soko hilo imepanda kutoka shilingi bilioni 416.0 mwaka 2021 hadi kufikia bilioni 847.3 mwaka 2024.

Kamishna wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware, alisema hayo Agosti 18, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi kati ya wahariri, waandishi wa habari na mamlaka hiyo.

Alisema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 103.7 katika kipindi cha miaka minne, likiwa ni wastani wa asilimia 26.3 kwa mwaka.

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu pekee, mitaji ya bima imeongezeka kutoka shilingi bilioni 906 hadi bilioni 993 kufikia Juni 30, 2025.

Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 9.5 ndani ya miezi sita.

Aidha, idadi ya watoa huduma wa bima imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi kufikia 2,425 Juni 2025.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 144.2 kwa kipindi hicho, ikiwa ni wastani wa asilimia 22.1 kila mwaka.

Dkt. Saqware alieleza kuwa ongezeko hilo limetokana na juhudi za serikali kupanua wigo wa huduma za bima nchini.

Amesema TIRA imeongeza aina mpya za watoa huduma, wakiwemo watoa huduma za afya (HSPs), warekebishaji na watengenezaji magari (ARMs), pamoja na watoa huduma wa kidigitali.

Pia, idadi ya kampuni za bima ya mtawanyo imeongezeka kutoka kampuni moja mwaka 2021 hadi kufikia kampuni nne mwaka 2024.

Katika sekta ya kilimo, Serikali imeanzisha konsortiamu ya bima inayojumuisha kampuni 15 kwa ajili ya kulinda wakulima dhidi ya athari za majanga ya asili.

Kamishna huyo alisema wakulima wa tumbaku mkoani Tabora tayari wamelipwa fidia kutokana na mvua kubwa, huku wakulima wa pamba wakilipwa baada ya kuathiriwa na wadudu waharibifu.

Kwa upande mwingine, Serikali imeanzisha pia konsortiamu ya mafuta na gesi, inayojumuisha zaidi ya kampuni 22 kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo muhimu inanufaika na fursa zilizopo nchini.

















PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY TORCH MEDIA