Arusha. Serikali imesisitiza kuwa hakuna leseni iliyotolewa wala itakayotolewa kwa ajili ya uchimbaji wa magadi soda ndani ya Ziwa Natron pamoja na tafiti kuonyesha wingi wa magadi hayo.
Pamoja na hilo imezitaka kampuni zinazotamani kuchimba magadi hayo, kufanya ubia na Kampuni ya Shirika la Maendeleo (NDC) kufanya uwekezaji huo katika eneo la Engaruka wilayani Monduli.
Kutokana na hilo, Kampuni ya Ngaresero Valley imeonesha nia ya kufanya uwekezaji wa magadi soda katika eneo hilo ikiwemo kuanzisha kiwanda cha kusindika kitakachotegemea uchimbaji ndani ya ziwa hilo.

Naibu Waziri wa Madini, Stephen Kiruswa
Awali Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Khalid Abdalah Rashid, alisema tafiti za upembuzi yakinifu zimekamilika na kampuni iko kwenye mchakato wa kupata vibali, ambapo mradi unatarajiwa kuzalisha zaidi ya tani 660,000 kwa mwaka.
Akizungumzia swala hilo, leo Agosti 18,2025 Naibu Waziri wa Madini, Stephen Kiruswa amesema kuwa eneo hilo liko chini ya Ramsar ambazo zinalindwa chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, na hivyo haliruhusiwi kwa uwekezaji wa aina hiyo.
“Hakuna leseni iliyotolewa na wala haiwezi kutolewa kwa ajili ya uchimbaji wa magadi ndani ya Ziwa Natron kwani ni eneo inayolindwa dhidi ya shughuli zote za uwekezaji hivyo hata uchimbaji zimepigwa marufuku” amesema.
Kiruswa ameiambia Mwananchi kuwa shughuli pekee inayoruhusiwa ni uokotaji wa asili wa magadi pembezoni mwa ziwa.

Viota vya ndege aina ya flamingo vilivyopo ndani ya Ziwa Natron, ambalo linatajwa kuwa eneo pekee barani Afrika linalotumika kwa mazalia makubwa ya ndege hao.
Aliongeza kuwa Serikali imeshaelekeza NDC yenye leseni halali ya uchimbaji kufanyia shughuli zake Engaruka, na si ndani ya Ziwa Natron, ili kuhifadhi ustawi wa ikolojia na kuendeleza makazi ya flamingo, ndege ambao kwa wingi wanapatikana pekee kaskazini mwa Tanzania.
“Hivyo kama kuna mwekezaji anataka kufanya uwekezaji kama huo awasiliane na NDC asiendelee kuhangaika na ziwa Natron” amesema.
Tamko la waziri linakuja baada ya jana viongozi wa serikali na viongozi wa mila kutoka vijiji tisa vinavyozunguka ziwa Natron kuitisha kikao cha dharura na kupinga mchakato wa maandalizi ya uanzishwaji wa mradi huo ndani ya Ziwa Natron.
Viongozi wa vijiji vya Engaresero, Pinyinyi, Gelai Lumbwa, Ichangiti Sapukin, Alaililai, Wosiwosi (Ngorongoro), na Magadini, Loondolwa Esirwa na Gelai Merugoi (Longido) walionya kuwa mradi huo unatishia mazingira, mifugo, kilimo na utalii.

Mwenyekiti wa vijiji tisa vinavyozunguka Ziwa Natron, Joshua Muriatoi Mollel, akizungumza kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza endapo mradi wa uchimbaji wa magadi soda utaanza kutekelezwa ndani ya ziwa hilo. Picha na Bertha Ismail.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijiji, Joshua Muriatoi Mollel, alisema si mara ya kwanza kufanyika jaribio la kuchimba magadi soda kufanyika ndani ya ziwa lakini kutokana na hatari zake kimazingira waliofanikiwa kusitisha.
Mtaalamu wa ndege na Mkurugenzi Mtendaji wa Nature Tanzania, Emmanuel Mgimwa, alisema uchimbaji wa magadi soda unaweza kuathiri flamingo kwa haraka zaidi.
“Idadi ya flamingo duniani imeshuka kutoka milioni 4.5–5 miaka mitano iliyopita hadi kufikia milioni 1.5–2 pekee ambapo Tanzania ndio ina utajiri wa zaidi ya asilimia 80 ya waliobaki na hii ni kutokana na kuharibiwa kwa mazingira yao ya kuishi na maeneo ya kuzaliana,” alisema.
Mgimwa aliongeza kuwa mradi huo ungehitaji mabadiliko ya mito inayopeleka maji ziwani, ikiwemo Mto Ewaso Ng’iro wa Kenya, jambo litakalovuruga usawa wa maji unaohitajika kwa flamingo kuzaliana.