Simba, kipa mpya ngoma imeiva!

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua jijini Cairo, Misri, lakini inaelezwa mabosi wa klabu hiyo wanapambana kumalizia dili na kipa mmoja kabla ya dirisha la usajili halijafungwa, na kinachoelezwa ni kwamba kuna sapraizi flani inaandaliwa ya kufungia.

Mastaa wa kikosi hicho wanaendelea kujifua huko Misri ikiwa ni siku chache baada ya kuondoka Ismailia walikotumia zaidi ya wiki mbili kuweka mambo sawa, huku wakizoweana kati ya wenyeji na wageni baada ya kutua kikosini hapo kwa mara ya kwanza.

Kinachoelezwa ni kwamba yule kipa wa JKT Tanzania, Yakoub Suleiman hatimaye mabosi wameamua kumfungia kazi kwa safari hadi Zanzibar kuzungumza na viongozi wa juu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), ambako ndiko iliko ajira yake, kwani jamaa ni askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi.

Inaelezwa kwamba kwa hatua iliyofikia Simba, suala la kipa huyo namba moja wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ lipo hatua nzuri na imebakiza vitu vichache ili kummiliki.

Mwanaspoti imepata taarifa za ndani kuhusu kipa huyo kusaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba, lakini ili uhalali ukamilike inatakiwa kutekeleza masharti iliyopewa na mchezaji kufanyiwa mchakato wa kupiga picha na kusafiri kwenda Misri mara tu baada ya kumaliza majukumu timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Chanzo hicho kimeiambia Mwanaspoti namna Simba inatakiwa kuzigawanya pesa za dau la usajili ambalo itatakiwa iweke JKU, JKT Tanzania na mchezaji mwenyewe, ikisemekana imepunguziwa kutoka Sh400 milioni na sasa inacheza katikati ya Sh300 milioni.

“Simba ilianza kuzungumza na JKT Tanzania baada ya kuona mambo hayapo sawa, walikwenda kuufuata uongozi wa juu wa JKU ambao umefanikisha jambo hilo na sasa mtihani umebakia kwao kutekeleza walichoambiwa,” kimesema chanzo hicho na kuongeza:

“Uongozi wa JKU utaitumia barua JKT TZ kuwaambia imemalizana na Simba, kwani hautambui mkataba mpya iliyomuongezea mchezaji huyo akisaini miaka miwili, kwa vile ilipaswa kurudi ofisini kwao ila hawakufanya hivyo, pamoja na hayo yote bado uongozi wa JKU umetoa mgawanyo wa pesa kwa JKT Tanzania.”

Simba ilipewa siku ya mwisho ya kuingiza pesa hizo Agosti 18, 2025 kama limekamilika hilo basi Yakubu katika safari ya kwenda kujiunga na kambi Misri ataongozana na kiungo mpya wa klabu hiyo, Neo Maema aliyesajiliwa kutoka Mamelodi Sundowns.

Yanga ilikuwa ya kwanza kuhitaji saini ya Yakoub kwa ofa ya Sh100 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu, jambo ambalo halikuwa na masilahi kwa mchezaji kwa sheria ya kazi yake ya askari wa JKU, kwani angegawana dau lake la usajili na ofisi yake hivyo angeambulia Sh50 milioni muda huo.

Kukamilika kwa usajili wa Yakoub aliyemaliza msimu uliyopita na ‘clean sheets’ nane, kunamuondoa Ally Salim kikosini anayetafutiwa timu ya kuichezea kwa mkopo msimu ujao au kuuzwa moja kwa moja.

Alipotafutwa Katibu wa JKU, Khatib Shadhil na kuulizwa suala hilo amesema: “Ni kweli jambo hilo linaendelea vizuri kwa pande tatu… kwa maana ya JKT Tanzania, JKU na Simba na lina asilimia kubwa ya kukamilika ila kwa sasa nikuambie tu bado halijakamilika.”