Taifa Stars ilistahili robo, ikikomaa inatioboa

KIKOSI cha Taifa Stars kimeandika historia mpya katika michuano ya CHAN 2024, baada ya kumaliza kileleni mwa kundi B kikiwa na pointi 10 kati ya 12, sawa na asilimia 83.33 ya pointi zote.

Suluhu dhidi ya Afrika ya Kati ilitosha kwa vijana hao wa Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuweka rekodi hiyo ya kibabe kwa mara ya kwanza katika mashindano ya CAF, kwani haijawahi kutokea.

Stars ilianza safari katika mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuichapa Burkina Faso mabao 2-0, kisha Mauritania 1-0, Madagascar 2-1 kabla ya juzi, Jumamosi kutupa karata yake ya mwisho katika hatua ya makundi.

Akiwa tayari na uhakika wa kucheza robo fainali ya CHAN, juzi kocha Morocco aliamua kupumzisha baadhi ya nyota wake muhimu, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Iddy Seleman ‘Nado’.

Morocco alifanya hivyo ili kutunza nishati ya wachezaji wake hao muhimu kwa ajili ya mechi ya robo fainali itakayochezwa Agosti 22, hata hivyo, hiyo ilikuwa fursa kwa Pascal Msindo, Lusajo Mwaikenda, Ibrahim Hamad Hilika wote kuanza kwa mara ya kwanza.

Mbali na hao, ilishuhudiwa pia Ahmed Pipino na Yusuph Kagoma ambaye alimaliza adhabu yake ya kadi mbili za njano wakicheza pamoja kwenye eneo la kiungo, na hayo haya ni mambo matano ambayo yameibaba Stars kumaliza kinara wa kundi B.

STAR 04

Siri ya kwanza ya Stars kumaliza kibabe hatua ya makundi ni ukuta wake.

Katika mechi mbili za kwanza, Stars ilicheza dakika 180 bila kuruhusu bao kabla ya nyavu zake kuguswa katika mechi ya tatu dhidi ya Madagascar, rekodi inayoweza kuelezewa kwa namba na nidhamu.

Wachezaji wa safu ya ulinzi kama Dickson Job na Ibrahim Hamad “Bacca” walionekana kuunganisha nguvu zao vizuri, huku mabeki wa pembeni Kapombe na Tshabalala wakisaidia mashambulizi bila kuacha mianya nyuma.

Kipa Yakoub Suleiman ambaye ameruhusu bao moja tu kwenye dakika 360 za mechi nne za hatua ya makundi alifanya kazi kubwa, akipangua mashuti ya wapinzani na kuongoza mstari wa nyuma kwa utulivu.

Kocha Hemed “Morocco” alijenga mfumo unaomlazimisha kila mchezaji kushiriki kwenye ulinzi kuanzia washambuliaji. Hii ilisababisha wapinzani kushindwa kupata nafasi nyingi za wazi.

Mechi dhidi ya Burkina Faso na Mauritania ni mifano halisi wapinzani walishindwa kulenga lango mara nyingi na hata walipojaribu, walikumbana na ukuta wa imara.

STAR 03

Hakuna kikosi kinachoweza kufanikiwa kwenye mashindano makubwa bila kuwa na viongozi, waswahili wanasema mtu mzima dawa.

Kwa Stars, jukumu hili limebebwa na Kapombe pamoja na Tshabalala.  Licha ya kwamba unaweza usiwaone na kitambaa cha unahodha wamekuwa wakifanya kazi kubwa uwanjani hata kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Mbali na uongozi wao kutokana na uzoefu wao, wamekuwa mfano hai uwanjani kwa kutoa zaidi ya asilimia mia moja ya mchango wao.

Wawili hao kila mmoja ameifungia Stars bao katika mashindano haya.  Bao la Kapombe liliifanya Stars kuibuka na ushindi dhidi ya Mauritania dakika za jioni kabisa huku Tshabalala akifunga kwenye mchezi ya kwanza ya mashindano dhidi ya Burkina faso.

Kapombe na Tshabalala wana zaidi ya muongo mmoja timu ya taifa na uzoefu wa michuano mikubwa, waliisaidia Stars kudhibiti presha kwenye dakika ngumu.

Uwepo wa wachezaji kama, Job ambaye ni nahodha, Bacca, Mudathir Yahya na Feisal Salum pia uliwapa vijana ujasiri. Hawa ni wachezaji waliopitia mazingira magumu ya mashindano ya kimataifa na kujua namna ya kudhibiti kasi ya mchezo.

STAR 01
STAR 01

Katika soka, kila mafanikio ya mashindano yanahitaji mtu wa kufunga magoli. Kwa Tanzania, jina hilo ni Clement Mzize. Kijana huyu amekuwa moto wa kuotea mbali, akionyesha ubora wa kumalizia mashambulizi na akili ya kusoma mchezo.

Katika mechi dhidi ya Madagascar, Mzize alipachika mabao mawili ndani ya dakika 20 za kwanza, jambo lililoweka Stars kwenye nafasi nzuri ya kutinga robo fainali mapema.

Uwepo wa mshambuliaji mwenye njaa ya ushindi kama Mzize umeongeza kasi kwenye safu ya mbele ya Stars. Wengine kama Iddy Nado na Abdul Suleiman ‘Sopu’ wamekuwa wakisaidia kwa kuwavuta mabeki wa wapinzani ili kumpa nafasi Mzize au washambuliaji wengine.

Kocha Morocco amethibitisha kwamba CHAN si tu kuhusu vipaji binafsi, bali pia mbinu na usomaji wa mchezo. Katika kila mechi, Morocco ameonyesha uwezo wa kufanya mabadiliko yanayoibeba timu.

Dhidi ya Mauritania, alicheza kwa uvumilivu akijua wapinzani watakuwa wakihesabu sekunde za kupata pointi.

Alisubiri hadi dakika za mwisho kuongeza nguvu ya kushambulia kwa kumwingiza mshambuliaji wa akiba,Nassor Saadun jambo lililosababisha presha kubwa na hatimaye Kapombe kufunga.

Dhidi ya Madagascar, mabadiliko ya mapema ya nafasi ya kiungo kwa kumtoa Hamza na kuingia Shekhan  yaliifanya Stars kuwa imara zaidi eneo hilo kutokana na kasi walipokuwa nayo wapinzani wao.

Morocco pia amekuwa akitumia vizuri mpango wa “pressing” yani kuusaka mpira kwa nguvu baada ya kupoteza hali inayowalazimisha wapinzani kukosea na kuipa Stars nafasi za haraka.

STAR 02

Stars imeonekana kama familia moja kila goli lililofungwa, kila mchezaji na benchi zima la ufundi wamekuwa wakifurahia pamoja.

Ari hii imetokana na maandalizi mazuri ya kabla ya mashindano, ambapo wachezaji walihamasishwa kwa malengo ya pamoja kuandika historia.

Benchi la ufundi limehakikisha kila mchezaji anajua nafasi yake na mchango wake kwa timu.

Umoja huu umeonekana hata katika lugha ya mwili uwanjani  wachezaji wakisaidiana, wakikumbatiana baada ya makosa na kushangilia kila hatua nzuri.

Hii ni ishara ya timu iliyojitolea kwa ajili ya nchi na sio mafanikio binafsi.

“Tulichoweka mbele ni nidhamu na mpangilio wa kiufundi. Hakuna kitu kinachokuja kwa bahati kwenye mashindano haya kila ushindi ni matokeo ya maandalizi, ushirikiano na nidhamu. Hii ni historia ya taifa, lakini bado safari haijaisha,” anasema Kocha Morocco.