TIKETI 10,000 zenye thamani ya Sh20 milioni, zimetolewa leo Agosti 18, 2025 na Benki ya NMB kwa ajili mechi ya robo fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kati ya wenyeji Tanzania dhidi ya Morocco.
Kiasi hicho kimetolewa kwa mfano wa hundi na Mkuu wa Idara ya Matawi ya benki hiyo, Donatus Richard na kukabidhiwa Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa sambamba na Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Donatus amesema lengo la kutoa kiasi hicho ni kuiunga mkono Taifa Stars inayokwenda kupigania nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
“Tunaipongeza Taifa Stars kwa rekodi ya kipekee, tunakuja kuunga mkono mambo mawili, la kwanza kwa mashabiki tutanunua tiketi elfu kumi na la pili kwa Stars tutaipatia kiasi cha Sh10 milioni kama bonasi,” amesema Donatus na kuongeza.
“Tunaamini kiasi hicho kitasaidia Stars kufanya vizuri kwenye mechi ya robo na tutahakikisha tunaendelea kuiunga mkono ili ifanye vyema zaidi.”
Kwa upande wa Msigwa, aliipongeza benki hiyo na kutoa wito kwa taasisi zingine kuiunga mkono Stars.
“Njooni tukaujaze Uwanja wa Mkapa, kwa wananchi mbali na tiketi hizi zilizonunuliwa endeleeni nanyi kununua kwa ajili ya kuujaza uwanja na kuipa sapoti Stars.
“Kama hatutaonekana uwanjani kipindi ambacho Tanzania tumepata fursa ya kuwa wenyeji hatutayatendea haki mashindano haya, hii isiishie kwa Chan, tunataka mashindano mengine kama All African Games yaweze kufanyika hapa sasa kama hatutaujaza uwanja huu kwa Chan itakuwaje hayo mengine,” amesema Msigwa.
Mchezo huo wa robo fainali utachezwa Ijumaa wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 usiku.