Uganda yaiduwaza Sauzi ikitinga robo CHAN 2024

MABAO mawili ya penalti ya dakika za majeruhi zimeibeba Uganda The Cranes kutinga robo fainali ikizifuata Tanzania na Kenya kama wenyeji kutunga hatua hiyo.

Uganda ilipata sare ya 3-3 mbele ya Afrika Kusini ambao walishindwa kuamini kama wameng’oka baada ya kuongoza kwa muda mrefu kipindi cha pili kabla ya kuongezwa dakika 8 zilizowatibulia.

Sare  iliyopatikana kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, jijini Nairobi umeifanya Uganda iliongoze Kundi C ikiwa na pointi saba.

Katika pambano hilo Uganda ilitangulia kupata bao dakika ya 31 kupitia kwa Jude Ssemugabi aliyemalizia pasi ya Patrick  Kakande.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko kabla ya kipindi cha pili Afrika Kusini kuchomoa kupitia kwa beki Ramahlwe Mphahlele
katika dakika ya 52 baada ya kipa wa Uganda, Joel Mutakubwa
kupangua vibaya mpira wa friikikii.

Dakika sita baadae timu hiyo iliongeza bao la pili kupitia Thabiso Kutumela aliyefunga kwa tobo mbele ya kipa Mutakubwa baada ya Sauzi kuanzisha mpira wa kurusha fasta na kufunga kirahisi.

Dakika ya 83 Ndabayithethwa Ndlondlo alifunga bao la tatu kwa shuti la mbali baada ya kipa wa Uganda kutoka kizembe langoni.

Hata hivyo, dakika tano baadae Uganda ilipata penalti kupitia kwa Allam Okello baada ya beki wa Afrika Kusini kufanya madhambi.

Wakati mashabiki wa Uganda wakikata tamaa na baadhi kutoka uwanjani kwa kuamini  timu yao imetolewa, timu hiyo ilipata penalti dakika ya sita kati ya nane zilizoongezwa baada mabeki wa Afrika Kusini kushika mpira katika piga nikupige.

Penalti hiyo ilitoamuriwa kwa msaada wa V.A.R kama ilivyokuwa ile ya kwanza ilifungwa na beki na nahodha wa Uganda, Rogers Torach.

Uganda imefuzu robo sambamba na Algeria ambayo ililazimishwa suluhu na Niger katika mechi nyingine iliyopigwa usiki huu jijini Nairobi ikifikisha pointi sita kama Afrika Kusini ili tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa ikiwatoa Wasauzi ambao walimwaga machozi mara baada ya mechi yao na Uganda.