Urais mwiba kwa vyama vya siasa

Moshi. Urais ni kaa la moto ndani ya vyama vya siasa nchini na mara nyingi kuleta mtafaruku!

Huu ndio mjadala unaoendelea kwa sasa baada ya makada wa vyama mbalimbali kuibuka hadharani na kupinga michakato ya uteuzi wa wagombea wao.

Kwa kuegemea uzoefu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 2015, Chama cha Mapinduzi (CCM) na sasa Chama cha ACT- Wazalendo kunatoa picha pana ya namna ugombea urais unavyokuwa kiini cha kuzusha migogoro.

Kwa upande wa upinzani sintofahamu inakuwa kubwa zinapojitokeza sura ngeni kuwaweka pembeni makada waliokuwa wamejiandaa na kuwa na uhakika wa kupitishwa kuomba kuwania nafasi hiyo huku CCM wakitafunana kutokana na makundi.

Hali inayofanya baadhi ya viongozi na wanachama kununa, wengine kususa kabisa huku wakiendeleza mijadala ya kupinga ama kukosoa taratibu za ndani za kuwapata.

ACT-Wazalendo kiongozi wake ngazi ya mkoa, Monalisa Ndala amedai kukiukwa kanuni za kumpata Lugaha Mpina kuwa mgombea urais.

Ndala amewasilisha barua ya malalamiko kwa katibu mkuu wa chama hicho.

Katika barua yake ya Agosti 14, 2025 kwenda kwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ndala alidai, Mpina hajakidhi matakwa ya kanuni za kudumu za uendeshaji wa chama toleo la 2015 hususan vifungu vya 16(4)(i), (iii) na kifungu kidogo cha (iv).

Vifungu hivyo vinataka awe mwanachama kwa muda usioupungua mwezi mmoja kabla ya kuteuliwa na chama na awe tayari kutangaza mali zake na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa na awe anaifahamu falsafa, itikadi na misingi ya chama.

Ndala alidai kanuni za uendeshaji wa chama hicho toleo la mwaka 2024 zinazohusu uchaguzi, sehemu ya 8(a) inamtaka mgombea awe mwanachama kwa kipindi kisichopungua siku saba kabla ya tangazo la uchaguzi.

Amesema kuwa, Mpina anakosa sifa kwa sababu alijiunga siku mbili tu kabla ya kuteuliwa na chama, hadi anateuliwa hakuna mahali popote ametangaza mali zake na alipaswa awe mwanachama siku saba kabla ya Aprili 18, 2025.

Leo Agosti 18, 2025 alipozungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, Ado Shaibu amesema mawasiliano hayo ni ya kawaida ya ndani.

“Nimeshangaa kuyaona nje. ACT-Wazalendo tuna uzoefu wa kuyashughulikia masuala hayo ndani na suala hili litashughulikiwa kwa njia hiyo,” amesema katibu mkuu huyo.

Amesema kwa chama chao, uteuzi wa mgombea urais ulishakamilika na fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi hiyo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ulishamakilika.

“Hatua tunayoendelea nayo ni kutafuta wadhamini. Tumefarijika na mwitikio mkubwa wa wananchi tangu tuanze programu hiyo jimboni Kisesa tarehe 16 Agosti 2025 na kisha kuendelea mikoa mbalimbali nchini.”

“Wale ambao wameshindwa hata kutekeleza matakwa ya katiba yao kwenye uteuzi wa wagombea urais wanajulikana, ni ishara ya wazi ya chama kinachoporomoka….,” amesema Shaibu.

CCM kuna makada wawili wamepinga mkutano mkuu wa Januari 18-19, 2025 uliompitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwania urais. Tayari suala hilo limefikishwa mahakamani na Dk Godfrey Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Wakati Dk Malisa akipeleka suala hilo kortini, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, licha ya kujiuzulu nafasi hiyo ya ubalozi akipinga uamuzi wa mkutano mkuu huo, ameendelea kukosoa masuala mbalimbali ndani ya chama.

Polepole aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM kwa sasa amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuzungumzia suala hilo akitaka viongozi waandamizi wa chama hicho kuzingatia kaiba na kanuni za chama.

Hata hivyo, makada na viongozi wa CCM, wamekuwa wakijibu wakisema mkutano mkuu wa CCM ndiyo chombo cha mwisho kwa uamuzi. Naibu Katibu Mkuu Bara wa CCM, John Mongella amewahi kusema mchakato wa kumpata Rais Samia ulizingatia taratibu zote za chama na hakuna tatizo.

Kinachoendelea sasa ndani ya ACT-Wazalendo na CCM, ni sawa na kilichotokea mwaka 2015 ndani ya Chadema, aliyekuwa katibu mkuu wake, Dk Wilbrod Slaa katikati ya mchakato wa uchaguzi mkuu huo alijiondoa ndani ya chama hicho.

Dk Slaa ambaye wakati huo Chadema ilikuwa inamwandaa kuwa mgombea urais, aliondoka akipinga mchakato wa kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (sasa ni  marehemu) kisha kumpitisha kuwa mgombea urais.

Lowassa aligombea urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama shirika vya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi, vilivyojulikana kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katikati ya vumbi hilo, mwenyekiti mwenza wa Ukawa na mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba naye alijiuzulu wadhifa wake huo miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, licha ya Dk Slaa na Profesa Lipumba kujiweka kando, Lowassa aliongoza upinzani kuendesha kampeni zilizokuwa na msisimko na mwisho wa uchaguzi, Ukawa ukashinda viti vingi vya madiwani, wabunge na kura za urais zikatofautiana kidogo.

Dk Magufuli wa CCM alipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.4 huku Lowassa akipata kura 6.07 milioni sawa na asilimia 39.97. Lowassa alijiunga Chadema baada ya jina lake kukatwa CCM kwenye kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais.

Mwaka 2020, fukuto kama hilo lilitokea CCM, kada wake mashuhuri aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika, Bernard Membe, alipoonesha nia ya kutaka urais kuchuana na Rais aliyekuwa madarakani, Dk John Magufuli.

Membe aliishia kufukuzwa ndani ya CCM, Februari 28, 2020. Aliamua kwenda ACT-Wazalendo alikopitishwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Katikati ya kampeni, chama hicho baadaye kilitangaza kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu. Hata hivyo, Membe aliendelea na msimamo wa kuwania urais na alifanya kampeni za kusuasua.

Kinachoendelea kwa sasa ndani ya CCM na ACT-Wazalendo kimekuwa na mitizamo tofauti kutoka kwa wanazuoni wakichambua hali hiyo na nini kinaweza kuwa sababu hususan kwa vyama va upinzani migogoro kuibuka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema kinachoonekana ni kama baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani hawajui wanachokitaka ni nini wala hawajui adui yao hasa ni nani na badala yake wanajipiga wenyewe risasi.

“Naona ni jinsi gani ambavyo upinzani unaendelea kujishoot (kujipiga risasi) mguuni. Yaani kwa mfano ukiangalia kinachotokea Chadema sasa hivi ni kitu ambacho kinatokea ndani au kwa maneno mengine kinaanzia ndani.

“Anatoka mwanachama anasema viongozi waliochaguliwa akidi haikutimia, halafu msajili anachukua hatua pamoja na kusitisha ruzuku. Wanatoka wanachama wengine wa Zanzibar wanasema mgawanyo wa mali si sawa wanafungua kesi,” amesema Dk Mbunda.

Amesema kutokana na hilo, ndiyo maana anaona upinzani unajipiga risasi wenyewe mguuni.

“Yaani kama watu ambao hawaelewi wanachokitaka ni nini na hawajui adui yao ni yupi, hawajui wanayeshindana naye ni nani katika hizi siasa.

Ni aidha pengine wanakubali kutumika maana saa nyingine kunakutumika vile vile kwenye siasa kwa masilahi binafsi kwa ajili ya kuvihujumu vyama vyao au hawajielewi wanachokitaka ni kipi hapo,” amesema Dk Mbunda.

Wakili mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa hatua ambayo suala hilo limefikia huku Mpina akiwa tayari amepewa fomu ya kuomba kuteuliwa, amesema msajili wa vyama vya siasa ndiye anayeweza kulishughulikia kwa kuwa anayo mamlaka.

Hii inatokana na ukweli kuwa kwa mujibu wa Sheria Vyama vya Siasa 2019 na marekebisho yake, msajili wa vyama vya siasa ndiye mwenye wajibu wa kuvilea vyama vya siasa na kama Ndala haridhiki, anapaswa kukata rufaa ngazi za juu.

“Hii haitofautiani sana na kilichofanywa na CCM, walipomteua Rais Samia Suluhu Hassan kupeperusha bendera yake. Mkutano mkuu ndio chombo cha mwisho na kwa mfano wa CCM, sidhani kama msajili anaweza kufanya chochote,” amesema wakili huyo.

“Msajili hapaswi kuwa na sura mbilimbili. Kama kweli ACT- Wazalendo wamekiuka katiba na kanuni zao, basi achukue hatua kama alivyochukua Chadema na pia aimulike pia CCM maana kuna wanachama wananung’unika,” amesisitiza.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa na kijamii, Florentina James amesema ukisikiliza hoja za Ndala zinaonekana zina mashiko hasa katika kigezo kinachomtaka mwanachama adumu kwa kipindi fulani kabla ya kuchaguliwa.

“Hili nadhani viongozi wa ACT- Wazalendo wanaweza kulitolea ufafanuzi vizuri kwa sababu kama kanuni ziko hivyo, kuna hoja, lakini kuna wengine wanasema hizo kanuni zilisharekebishwa. Viongozi ndio wanatakiwa waliongelee hili,” amesema.

Hata hivyo, amesema anachokiona, chuki ndani ya vyama wakati wa uteuzi wa mgombea urais unasababishwa na wanachama wenye matamanio na ambao wamejiandaa kwa muda mrefu lakini badala yake wananyang’anywa tonge mdomoni.