Tanga. “Tunakutana na nyoka na wadudu wengine hatari, tunachomwa na miba na visiki,” anasimulia Mashabani Mchelo, mkazi wa Handeni Mjini, mkoa wa Tanga.
Anasema safari ya kwenda porini kutafuta kuni huchukua kati ya saa mbili hadi tatu kwenda na kurudi, na mara nyingine zaidi ya hapo kutokana na ugumu wa upatikanaji wa kuni.
Mashabani, anayeishi kijiji cha Kwamasaka, anaeleza kuwa changamoto hizi ni sehemu ya maisha ya kila siku. “Bila kuni huwezi kupika, hivyo ni lazima kuamka asubuhi na mapema kwenda msituni, jambo linalosababisha shughuli nyingine za kiuchumi kusimama,” anaeleza.
Hata hivyo, anaongeza kuwa msituni nako kuna hatari kubwa, kwani wanaweza kukutana na nyoka na wadudu wenye sumu, japo hakuna kesi anayokumbuka hivi karibuni. Anasema iwapo mtu atang’atwa bila msaada wa haraka, maisha yake huwa hatarini.

“Pia, mara nyingine tunajiumiza kwa kujikata kwa panga, kuchomwa na visiki au kuanguka kwenye mashimo yaliyofichika,” anasema mama huyo, akionyesha jeraha bichi linalovuja damu alilopata muda mchache uliopita.
“Changamoto nyingine zinagusa hata maisha ya kifamilia. Ukichelewa kurudi na kuni, mumeo anaweza kuudhika kwa sababu ya njaa na ikawa chanzo cha ugomvi au hata kuvunjika kwa ndoa kwa wivu wa kwanini umechelewa,” anasema Mashabani.
Mkazi mwingine wa mtaa wa Vibaoni, wilayani Handeni, Fatuma Mohamedi, anataja changamoto hizo, akiongeza nyingine ya kukimbizwa na walinzi waliopo kwenye misitu ya hifadhi, maeneo ambayo hayaruhusiwi kufanya uvunaji wa miti bila kibali.
Anasema katika harakati hizo yapo madhara yanayoweza kutokea, ikiwemo kudondoka wakati wa kukimbia na mtu kuingia kwenye kisiki kikamchoma na kupoteza maisha, au kuvunjika endapo atadondoka ghafla wakati wa kukimbia walinzi wa hifadhi.
Fatuma anasisitiza licha ya changamoto hizo wanalazimika kuendelea na shughuli hizo kwa sababu nishati nyingine ambazo zinatajwa kuwa mbadala ni za gharama na hawawezi kumudu.
“Mtungi wa gesi kujaza ni Sh25,000, wengi hatuwezi kumudu gharama hiyo, ndio sababu sisi wengine tunatumia kuni na mkaa,” anasema.
Mama huyo anaongeza kuwa, “… kama nia ya Serikali ni wananchi tutumie nishati safi, bei ishushwe na kuangalia ile inayoweza kuwa rafiki kwa kila kundi. Bila kufanya hivyo, kwa maeneo ya pembezoni bado itakuwa ni mtihani kwao kufanya mabadiliko.”
Anaongeza kuwa hakuna asiyetaka kutumia nishati ya gesi katika shughuli zake, kwani ina faida nyingi, ikiwemo kuokoa muda wa mapishi, mazingira safi kwa mpishi, lakini pia hata kiafya nishati hiyo haina moshi wa kukera kama kuni na mkaa, ila suala la gharama ndiyo kikwazo.
Kundi jingine la watumiaji wakubwa wa kuni katika wilaya hii ni wafanyabiashara wa chakula, hasa wanaokaanga viazi maarufu chips, kwani biashara zao hufanyika kila siku na kwa muda mrefu.
Mfanyabiashara wa kuuza chips, Ali Kisuse, anasema hajawahi kufikiria kutumia gesi kutokana na mazingira ya kazi pamoja na gharama kubwa za nishati hiyo.
Akifafanua, Ali anasema vibanda vyao vipo maeneo ya wazi na pembezoni mwa barabara, jambo linalosababisha upepo kuwa mwingi. Hali hiyo, ameeleza husababisha moto wa gesi kutotulia na mtungi kuisha haraka, hivyo kuongeza hasara kwao.
“Wengi wetu tunafanya biashara kwenye mabanda yaliyo nje ya nyumba. Mazingira haya si rafiki kwa matumizi ya gesi kwa sababu ya upepo, jambo linaloweza hata kusababisha hatari. Tunahitaji elimu ya namna ya kutumia miundombinu ya gesi bila madhara, lakini wengi tunaogopa, ndiyo maana hatujatumia,” anasema Ali.
Kwa sasa, wafanyabiashara hao hutegemea vumbi la mbao kama nishati ya kupikia. Wananunua kwa kati ya Sh1,000 hadi Sh2,000 kwa kiroba la kilo 50, na kwa mwezi hutumia kati ya Sh30,000 na Sh60,000, gharama wanayoona kuwa nafuu kwao.
Ali anaeleza kuwa nishati ya gesi bado ni ghali. “Mtungi wa gesi hujazwa kwa Sh24,000, lakini matumizi yake hayafiki wiki moja. Kwa kazi hii, sidhani hata kama siku itaisha kwa mtungi wa gharama hiyo. Hii inaweza kufanya gharama ya mwezi kuwa zaidi ya mara mbili ya faida tunayopata, hivyo siyo biashara yenye tija kwetu,” anasisitiza.
Mtazamo wa viongozi wa mtaa, wilaya
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kileleni, Kisaga Mbalu, eneo linalohusiana na hifadhi ya Mlima Mhandeni maarufu kwa uvamizi wa watu wanaokata kuni na mkaa, anasema changamoto zinazotajwa na wananchi kuhusu nishati safi ni sehemu ya matatizo makubwa yanayoikumba jamii ya Handeni.
“Tunajitahidi kutoa elimu ya matumizi ya gesi na utunzaji wa misitu kwa kupanda miti, lakini bado kikwazo kikubwa ni gharama na upatikanaji wa gesi. Kila mwananchi ukiuliza anakiri anapenda kutumia nishati safi, ila kipato chao na bei ya gesi ndiyo tatizo,” anasema Kisaga.
Anaeleza kuwa uongozi wa mtaa unahamasisha vikundi vya wanawake kuungana na kununua vifaa vya gesi kwa pamoja ili kupunguza gharama. Kwa njia hiyo, wananufaika pia kwa kupata misaada kupitia vikundi, huku jukumu lao likibaki kujaza mitungi ya gesi.
Kisaga anasema pia Serikali ya Mtaa wa Kileleni inatoa elimu ya utunzaji wa misitu na madhara ya matumizi ya kuni na mkaa, elimu ambayo hutolewa na wataalamu kutoka idara ya afya na misitu.
“Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, mtaa wa Kileleni una wananchi 2,400, sawa na kaya 700. Kati ya kaya hizo, 470 zinatumia gesi. Elimu inaendelea kutolewa ili kunusuru misitu ya hifadhi iliyopo maeneo haya,” anasema Kisaga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, anasema uelewa wa wananchi kuhusu nishati safi umeongezeka, kwani wamepunguza uvunaji wa misitu na kuongeza matumizi ya gesi.
“Kwanza tuliwahamasisha wananchi na taasisi kuona umuhimu wa kutunza mazingira yao, kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, na badala yake kurudi kwenye matumizi ya gesi. Mafanikio yanaanza kuonekana. Magereza ya wilaya ya Handeni na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) yameanza kutumia gesi kwenye mapishi yao. Hii ni hatua kubwa kwetu na tunajivunia,” anasema Nyamwese.
Anaongeza kuwa licha ya mafanikio hayo, bado juhudi zinaendelea, lakini tayari idadi ya wananchi wanaoomba vibali vya kuvuna misitu kwa ajili ya kuni na mkaa imepungua ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita.
Hadi sasa, wilaya ya Handeni imefanikiwa kutenga hekta 1,060 za misitu kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa endelevu katika vijiji vya Gendagenda na Mkalamo, huku kukiwa na misitu ya vijiji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 32,000.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917