Geita. Vijana 12,000 kutoka mikoa ya Geita, Kagera, Tabora na Tanga wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kuwawezesha kiuchumi unaotekelezwa katika maeneo yaliyopitiwa na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Mradi huo ni sehemu ya mpango wa uwajibikaji wa kampuni hiyo kwa jamii wakati na baada ya ujenzi wa bomba hilo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika leo Agosti 18, 2025 katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema mradi wa bomba la mafuta utasaidia vijana kukabiliana na changamoto za ajira na kipato zinazowakabili.

Amesema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kukamilika Julai 2026 huku Serikali ya Tanzania ikiwa tayari imetoa Sh1.125 trilioni.
Dk Biteko amesema kupitia mradi huo, kampuni 200 za Kitanzania zimeajiriwa na fedha zinazopatikana zinazunguka kwenye maisha ya kawaida ya Watanzania hasa wale wanaojishughulisha na kazi za kawaida.
“Miradi kama hii si manufaa ya mradi pekee, bali ni namna wananchi wanavyonufaika kutokana na uwepo wake, zaidi ya kampuni za Kitanzania 200 zimeajiriwa na fedha zinazozunguka zimewanufaisha wananchi wa kawaida wakiwamo mama ntilie na bodaboda,” amesema Biteko.
Kaimu Mkurugenzi wa EACOP, Godfrey Mponda amesema tangu mwaka 2024, vijana 170 wameajiriwa moja kwa moja, 110 wako masomoni na 238 wanasomeshwa kupitia mpango huo ili baadaye watumie ujuzi kwa maendeleo ya nchi.
Amesema bomba hilo linalojengwa kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga, lina urefu wa kilometa 1,443 huku kilometa 1,147 zikiwa Tanzania na kilometa 296 Uganda.
Meneja wa Uwajibikaji na Uwekezaji kwa Jamii wa EACOP, Clare Haule amesema tangu kuanza kwa kampuni hiyo, miradi ya maji, barabara, elimu na afya imetekelezwa, pamoja na mradi huo wa kuwawezesha vijana kiuchumi katika mikoa ambayo bomba hilo linapita.

Amesema vijana wengi wanakumbana na vikwazo vingi kama ajira, ukosefu wa mafunzo stadi, ugumu wa kupata mitaji na katika kukabiliana na changamoto hizo, kampuni inaenda kutekeleza awamu ya kwanza ya mradi wa kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa mikoa minne ya awali huku mikoa mingine iliyobaki ikisubiri awamu ya pili ya utekelezaji.
“Miradi hii inaenda kutatua changamoto hii kwa kutoa ujuzi unaolingana na mahitaji ya soko, kuboresha huduma za kifedha na kuondoa vikwazo vya ujasiriamali na ajira binafsi,” amesema Haule.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi amesema mradi wa bomba la mafuta ni sehemu ya miradi ya kimkakati unaotekelezwa na Serikali na wabia mbalimbali.
“Mradi huu umekuwa na manufaa mengi makubwa kulikuwa na changamoto kubwa ya ajira, lakini miradi hii ya kimkakakti imeendelea kupunguza tatizo hilo tayari Serikali imetengeneza sera na sheria za kuwasaidia vijana kupata mitaji na fursa za ajira ili wanufaike moja kwa moja na miradi iliyopo nchini,” amesema Katambi.