Wanaocha shule nchini wapungua, mikoa hii bado

Dar es Salaam. Wakati wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wanaoacha shule wakipungua kati ya mwaka 2022 hadi 2024, mikoa ya Tabora, Geita, Mwanza na Kagera bado ngoma ngumu.

Ripoti ya Best Education ya mwaka 2025 iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inaeleza kuwa idadi ya wanafunzi walioacha shule kwa kipindi husika ilipungua kutoka 193,605 waliokuwapo mwaka 2022 hadi kufikia 139,192 mwaka 2024, ikiwa ni sawa na pungufu ya asilimia 28.10.

Kwa sekondari, idadi ya wanaoacha shule ilipungua kwa asilimia 25.9 kutoka wanafunzi 136,313 waliokuwapo mwaka 2022 hadi kufikia wanafunzi 100,998 mwaka 2024.

Wakati ahueni ikionekana, mikoa hiyo minne bado inahitaji kazi ya ziada ili kuhakikisha wanafunzi wanaoanza shule wanamaliza kwa idadi inayotakiwa kwa ngazi zote.

Mikoa hiyo, kwa ngazi ya elimu msingi, inabeba asilimia 44.7 ya wanafunzi wote walioacha shule mwaka 2024 na asilimia 28.98 ya wanafunzi wote waliokacha shule ngazi ya sekondari mwaka 2024.

Akizungumzia suala hili, mtafiti wa elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema ni vyema ukafanyika utafiti katika mikoa husika ili kubaini vyanzo vya changamoto hiyo ili vishughulikiwe.

Mbali na tafiti hiyo, ametaka kuangaliwa upya gharama zinazotumiwa na wazazi hadi kumpeleka mwanafunzi shule, kwani jamii kubwa inashindwa kuzimudu, hali inayofanya wanafunzi wengi kuacha shule na wengine kulazimika kuingia katika shughuli za kujiingizia kipato.

“Nadhani ni wakati muafaka sasa wa kuja na mpango kabambe wa kuangalia namna ya kuzisaidia kaya maskini kuwapeleka watoto shule kupitia Tasaf. Tunaweza kuangalia kiwango cha fedha kitakachowasaidia kununua mahitaji yao ili waende shule, kwa sababu kuna kaya nyingi zimeshindwa hili,” amesema.

Hilo lifanyike wakati jitihada za kuongeza mtazamo wa jamii juu ya umuhimu wa elimu zinaongezwa, hasa katika kipindi hiki ambacho elimu inaonekana kukosa umuhimu baada ya wanaomaliza kukosa ajira.

“Kukosekana kwa ajira kunafanya wazazi na watoto kuona elimu haina umuhimu. Bora waingie katika shughuli za kiuchumi kama kilimo, madini na uvuvi, ambapo wanapata fedha ya haraka tofauti na wao kukaa darasani. Hili linafanya hata ambao hawakuacha shule kuvutwa na mafanikio ya wengine,” amesema Nkoronko.

Kwa upande wa wanafunzi, ametaka wakumbushwe juu ya umuhimu wa elimu na namna itakavyowasaidia baadaye katika maisha yao ya kila siku.

Mimba za utotoni na ndoa pia ni jambo ambalo alilogusia, kwani bado kuna jamii ambazo zinaruhusu wasichana wakiwa katika umri mdogo kuolewa baada ya kupata mimba, ikiwemo katika mikoa hiyo.

“Mwanafunzi akipata ujauzito inakuwa rahisi kuolewa, na hapo ndiyo tunapata ndoa za utotoni. Tukiweza kudhibiti haya, tunaweza kuchangia watoto kukaa shuleni,” amesema Nkoronko.

Kuhusu uwezeshaji kaya kiuchumi, alilosema Nkoronko pia liliungwa mkono siku chache zilizopita, ambapo wadau wa elimu wakiwamo wazazi na walezi wameshauri kuwapo mpango wa Taifa wa kuangalia wanafunzi wanaotoka familia zisizojiweza ili kuwasaidia kufikia ndoto zao kielimu.

Hiyo ni kutokana na uwepo wa wanafunzi wanaoishi maisha magumu, wakiwamo wenye uhitaji maalumu wanaoishi na walezi au wazazi wasioweza kumudu mahitaji ya shule, hasa vifaa kama madaftari na sare.

Ambangile Mwanyembe, mmoja wa wazazi kutoka jijini Mbeya, amesema licha ya Serikali kutangaza elimu bure, bado zipo familia zenye kipato duni hadi kushindwa kumudu mahitaji ya wanafunzi, akiomba kuwapo mkakati maalumu kuwafikia wenye uhitaji.

Amesema kama inavyofanyika kwa elimu ya juu kwa kutoa mikopo, mpango huo unaweza kufika hadi elimu ya msingi ambayo ndiyo muhimu zaidi kwa maisha ya binadamu katika shughuli za kila siku.

“Pengine naweza nisieleweke, lakini ukweli ni kwamba kuna wazazi na walezi kipato chao ni duni kumudu mahitaji ya wanafunzi. Niombe Serikali, kwa dhamira yake ya elimu bure, mikopo au ufadhili uanze kwa shule za msingi, ambapo elimu hiyo ndiyo muhimu zaidi,” alisema Mwanyembe, Julai 22 mwaka huu.

Jambo hilo liliungwa mkono na Ofisa Elimu Kata ya Iyela jijini Mbeya, Nsajigwa Mwakapala, aliyesema mwanafunzi kukosa mahitaji ya darasani anakosa utulivu na kumshusha kitaaluma, akiomba wadau kuendelea kujitolea kuwagusa wenye uhitaji.

“Tunaendelea kuishauri Serikali iwafikie wanafunzi wenye uhitaji, ikiwamo mikopo kwa ngazi za msingi, lakini nawapongeza wadau wanaojitolea kusaidia wanafunzi wenye mazingira magumu,” amesema.

Kuhusu kukosekana kwa ajira kunavyokatisha morali ya wanafunzi kuendelea na shule, Serikali imeweka mkakati kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Taifa ya Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipokuwa akizungumza na wahariri Julai mwaka huu, alisema wakati wa utekelezaji wa Dira 2025, ukuaji wa uchumi ulikuwa kwa wastani wa asilimia 6.2 hadi asilimia 6.7, ambao mashirika ya kimataifa yaliusifia, lakini ukuaji huo haukuwa jumuishi vya kutosha kwa kiwango kilichopangwa.

Hiyo ni kwa sababu kasi ya upunguzaji umaskini na utengenezaji wa ajira haukuwa kwa kiwango unavyotakiwa.

Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mhariri wa Nipashe, Salome Kitomari, aliyehoji ni kitu gani ambacho Serikali ilijifunza katika utekelezaji wa Dira 2025, wakati ikielekea utekelezaji wa Dira 2050.