WATAALAM WANAOSIMAMIA UAANDAAJI NA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI WAASWA KUTUMIA KIKAMILIFU MFUMO WA CBMS

Kamishna wa Bajeti, Wizara ya Fedha, Bw. Meshack Anyingisye, akizungumza wakati akifungua Kikao kazi cha Wataalam wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa, katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma, kuhusu Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS), ambapo aliwasihi kutumia mafunzo hayo kama fursa katika kubadilisha utendaji katika usimamizi wa Bajeti ya Serikali.

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Bajeti Wizara ya Fedha, Bw. Fundi Makama, akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kikao kazi cha Wataalam wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa, kuhusu Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS), kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Bajeti Wizara ya Fedha, Bi. Tunsume Mlawa, akitoa mafunzo kuhusu Waraka wa Hazina Namba moja mwaka 2025/26 kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, wakati wa kikao kazi cha Wataalam wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Baadhi ya Washiriki wa Kikao kazi cha Wataalam wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa, wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yanatolewa kuhusu Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS), kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.

Kamishna wa Bajeti, Wizara ya Fedha, Bw. Meshack Anyingisye (Katikati aliyeketi), na Makamishna wasaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Bajeti Wizara ya Fedha, Bw. Fundi Makama (kushoto aliyeketi) na Bi. Vicky Jengo (kulia aliyeketi), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Kikao kazi cha Wataalam wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa, kuhusu Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS), kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)

…………….

Na. Josephine Majura na Joseph Mahumi WF, Dodoma

Wataalam wa wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali wameagizwa kutumia mafunzo ya Mfumo ulioboreshwa wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS), kuboresha utendaji kazi katika usimamizi wa uandaaji na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Kamshina wa Bajeti, Wizara ya Fedha, Bw. Meshack Anyingisye wakati akifungua mafunzo ya Mfumo wa CBMS ulioboreshwa na baadae kufanya Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2024/25, Maandalizi ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2025/26 na kupata maoni ya kuboresha mchakato wa maandalizi ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2026/27.

Bw. Anyingisye alisema wataalam hao ni watu muhimu sana katika uandaaji na utekelezaji wa bajeti ya Serikali hivyo watumie mafunzo hayo kusimamia bajeti na kushauri Idara tumizi namna bora ya kutekeleza bajeti zao pamoja na kuboresha usimamzi wa bajeti ya Serikali.

“Usimamizi wa bajeti sio jukumu la Wizara ya Fedha tu, ni jukumu la kila mmoja wetu hivyo ni vema tukatekeleza majukumu yetu kikamilifu katika kushauri na kuchakata takwimu mbalimbali kutoka katika bajeti zetu”, alisisitiza Bw. Anyingisye.

Aidha, alisisitiza kuwa ushiriki wa watumishi hao katika kikao hicho unaashiria kujitolea kwa pamoja katika kuboresha utekelezaji na usimamizi wa bajeti ya Serikali, kuongeza ufanisi katika mchakato wa bajeti na kuhakikisha vipaumbele vya Serikali vinatekelezwa ipasavyo.

Awali akizungumzia mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi wa Bajeti anayeshughulikia uchambuzi na mbinu za kibajeti Wizara ya Fedha, Bw. Fundi Makama, alisema mafunzo hayo yamehusisha wadau kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Alisema mafunzo hayo ya siku tano (5) yatatolewa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusu mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa na awamu ya pili itajikita kwenye Tathmini ya Uandaaji wa Bajeti ya 2025/26 na tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya 2024/25. 

Bw. Makama alibainisha kuwa mafunzo hayo yatawezesha kupata maoni ya mchakato wa maandalizi ya Mwongozo wa uandaaji wa Mpango na Bajeti ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa upande wake Bw. Deodatus Kayango, Katibu Tawala Msaidizi wa Mipango na Uratibu kutoka Mkoa wa Geita, ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo alisema mafunzo hayo yatawezesha kufanya mipango yao kwa kutumia mifumo hali ambayo inatarahisisha upangaji, utekelezaji na tathmini ya mipango hiyo.

Kikao kazi cha wataalam wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa ni jukwaa muhimu la kutafakari na kujadili kuhusu mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25, uandaaji wa bajeti ya 2025/26 na kupata maoni ya maandalizi ya  Mwongozo wa uandaaji wa  Mpango na Bajeti ya Serikali wa mwaka 2026/27 ili kubaini maeneo ya kuboresha na kuweka mikakati itakayosaidia kuboresha uandaaji wa mipango na bajeti kwa mwaka 2026/27.