Watengeneza ajali ili walipwe bima kukiona cha moto

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha huduma za bima zinatolewa kwa haki nchini, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), imeonya baadhi ya watu wenye tabia ya kutengeneza matukio ya ajali ili walipwe zaidi ya haki ya kile kinachowastahili ikisema ni kosa kisheria na wakibainika watatupwa jela.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Bima, Dk Baghayo Saqware leo Jumatatu, Agosti 18, 2025, kwenye mkutano wa waandishi na wahariri wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, ukiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu sekta nzima ya bima, kueleza mafanikio na muelekeo wa mamlajka hiyo.

Kamishna wa Bima Dk Baghayo Saqware akizungumza mbele ya waandishi na wahariri wa vyombo vya habari leo Agosti 18, 2025.

“Kuna matukio ya ajali za kutengeneza ni hatari kwa kuwa ni kosa la jinai na utafungwa jela si chini ya miaka mitatu.

“Tumeanzisha kitengo cha uchunguzi wa bima kwa ajili ya kesi zenye shaka uchunguzi wa kipolisi utaanza mara moja na watakaobainika wataingia kwenye makosa ya jinai au ya kiuchumi,” amesisisitza.

Sambamba na hilo, kwa watoa huduma nao wanapaswa kutoa huduma kwa haki na ndani ya muda huku mamlaka hiyo ikiwataka kuacha janjajanja za kukwepa malipo.

“Kampuni za bima zinapaswa kulipa kwa wakati na usahihi mteja yeyote asidhulumiwe bima yake kwa sababu ni kubwa na ni haki yake, tukumbuke kuna watu wanaongeza chumvi na hatutaki mtu alipwe zaidi ya wanavyostahili,” amesisitiza.

Akizungumza alipotafutwa na Mwananchi, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano amesema ikitokea watu wachache wanaghushi au kutoa hongo ili kulipwa zaidi inaleta changamoto ya gharama jambo linalotengeneza mzigo usiostahili kwa kampuni husika na matokeo yake kuelemewa hata kushindwa kuwalipa wadau wengine.

Katika hatua nyingine, Tira imesema viwango vinavyotakiwa kulipwa katika huduma ya bima ya afya kwa wote vipo karibu kutangazwa na Waziri wa Afya.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni baada ya miaka takribani ya 12 ya vuta nikuvute ya mchakato wa Bima ya Afya kwa Wote ukihusisha kwenda na kurudi bungeni kutokana na unyeti wake hadi pale ilipoanza Januari mosi 2025.

Ikumbukwe, mwaka 2024, Serikali kupitia Wizara ya Afya iliandaa na kupitisha Kanuni za Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha utekelezaji wa sheria hiyo. Kanuni hizo zimeweka misingi ya utekelezaji, usimamizi na ushirikishwaji wa wadau katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya bima ya afya kwa kila Mtanzania.

“Tumepitia vitita vyote vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), bado waziri hajatoa viwango vinavyotakiwa kwenye kanuni tumejadiliana naye kile kiwango cha standard ambacho mwananchi anaweza kulipa tupo kwenye hatua za mwisho kabisa kutangaza na atakayetangaza ni Waziri wa Afya,” amesema Kamishna huyo.

Baada ya kupewa majukumu ya kupitia vifurushi vya NHIF kuanzia mwaka huu Kamishna Saqware amesema wanapitia kimoja baada ya kingine na vipo vilivyoidhinishwa na vingine wanaendelea kuboresha.

“Kuna usimamizi wa hivyo viwango sio tu NHIF wanatoa inabidi tukae na wizara sisi Tira wadau wa afya na wananchi,” amebainisha.

Akieleza kuhusu huduma kwa mtu mwenye kadi ya bima amesema inapaswa kuwa sawa sawa na mtu anayelipa pesa taslimu.

Msingi wa kuzungumza hilo unatokana na hoja iliyoibuliwa na mmoja ya washiriki wa mkutano huo juu ya madai ya uwepo wa huduma isiyostahili kwa wale wenye kadi ya bima ikiwa ni tofauti na wenye pesa.

“Tumeanza kuwasajili watoa huduma za afya huku wakitoa ahadi ya kuwahudumia wenye kadi kama wanavyohudumiwa wenye pesa taslimu.

“Zamani kabla Mamlaka haijaingizwa kwenye huu mfumo watoa huduma za hospitali walikuwa wanatoa huduma lakini hawadhibitiwi. Tukaona changamoto hii na matarajio yetu ukipata tatizo la kuhudumiwa tofauti tuwanyang’anye kazi ya kuhudumia watu wenye kadi abaki na watu wa keshi,” ameeleza.