Zanzibar. Ili kukuza uchumi wa kidijitali, upanuzi wa huduma za mtandao Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar (WUMU), Khalid Salum Mohammed amesema ni muhimu kuwe na ushirikiano zaidi kati ya sekta binafsi na umma.
Amesema hayo baada ya Kampuni ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) kutia saini makubaliano ya ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuharakisha mageuzi ya kidijitali Zanzibar, na kupanua upatikanaji wa huduma bora katika visiwa hivyo.
“Ushirikiano huu kati ya Airtel Tanzania na ZICTIA ni hatua muhimu katika utekelezaji wa miradi ambayo itaongeza ujumuishi wa kidijitali kwa wananchi wetu,” amesema.
Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa ubia kati ya sekta binafsi na ya umma akieleza: “Tunaamini katika ubia wa sekta ya umma na binafsi si kama sera tu, bali kama njia ya kivitendo ya kuharakisha e-serikali, e-elimu, e-afya na e-biashara, hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa vya kutosha.”
Makubaliano hayo yaliyosainiwa hivi karibuni Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, amebainisha makubaliano hayo yanaendana na ajenda ya serikali ya kidijitali na malengo mapana ya ujumuishi wa kijamii na kiuchumi.
“Mkataba huu unaonyesha dhamira ya Airtel kuwa zaidi ya kampuni ya mawasiliano, tunawekeza kwenye miundombinu na ushirikiano unaowezesha jamii, kusaidia vipaumbele vya Serikali na kuiweka Zanzibar kwenye njia ya ukuaji shirikishi na ubunifu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Shukuru Awadh Suleiman amesema ubia huo unaonyesha nafasi kubwa ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufungua fursa za sekta ya Tehama Zanzibar.
“Kwa kupitia ushirikiano huu, tunapanua mtandao wetu wa miundombinu na kuunda jamii iliyounganishwa zaidi ambapo wananchi, wafanyabiashara na taasisi za Serikali watanufaika na huduma za kidijitali zilizo salama, zenye uwezo mkubwa na za kuaminika,” amesema.