Arajiga aandika historia kwa kadi nyekundu CHAN 2024

Jana refa Ahmed Arajiga alichezesha kwa mara ya kwanza mechi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) ambapo alikuwa refa wa kati wa mchezo baina ya Algeria na Niger katika Uwanja wa Nyayo, Nairobi Kenya.

Mchezo huo ulimalizika kwa matokeo ya sare tasa ambayo yameifanya Algeria kuungana na Uganda kufuzu robo fainali ya mashindano hayo.

Hata hivyo kuchezesha mashindano hayo kwa mara ya kwanza hakujamzuia Arajiga kuonyesha makali yake ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara hasa kwa wachezaji watovu wa nidhamu na wale wanaopenda kucheza faulo.

Makali ya Arajiga jana yalikuwa mwiba kwa Niger ambayo ilijikuta ikimaliza mechi hiyo ikiwa pungufu baada ya mchezaji wake Ibrahim Djingarey kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 77.

Kabla ya hapo, Djingarey alionyeshwa kadi ya njano na Arajiga katika dakika ya 47 baada ya kucheza faulo na dakika 30 baadaye akafanya faulo nyingine iliyopelekea aonyeshwe kadi ya njano ya pili na kufanya aonyeshwe kadi nyekundu.

Arajiga amekuwa refa wa tano kuonyesha kadi nyekundu katika Fainali za CHAN 2024 akifuata nyayo za Sharmirah Nabadda, Jelly Chavane, Brahamou Sadou Ali na Vincent Kabore.

Nabadda kutoka Uganda alimuonyesha kadi nyekundu Andriamirado Andrianarimanana wa Madagascar katika mechi ya timu yake dhidi ya Mauritania.

Refa Brahamou Sadou Ali alimuonyesha kadi nyekundu mchezaji wa Kenya, Marvin Omondi katika mchezo baina ya timu yake na Angola uliochezwa Agosti 7, 2025.

Agosti 10, 2025, Refa Vincent Kabore alimuonyesha kadi nyekundu, Chrispine Erambo wa Kenya baada ya kumchezea rafu mbaya mchezaji wa Morocco.

Baada ya hapo akafuata Chavane ambaye alimuonyesha kadi nyekundu Abdoulaye Toure wa Burkina Faso katika mchezo dhidi ya Mauritania.