WAKATI Simba ikimnasa nyota kiraka Naby Camara kutoka Guinea na wakali wengine wakiendelea kujifua huko Cairo, Misri, Mwanaspoti limedondoshewa faili la siri namna beki kitasa wa Wekundu hao alivyopitiwa na aliyekuwa kocha mkuu wa zamani wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha.
Benchikha aliwahi kuinoa Simba kwa kipindi kifupi misimu miwili iliyopita kabla ya kuondoka mara baada ya Wekundu hao kupoteza mechi ya marudiano ya Dabi ya Kariakoo mbele ya Yanga na kutua JS Kabylie ya Algeria, japo kwa sasa ameshaachana nayo na kutua zake USM Alger.
Sasa inadaiwa kocha huyo ndiye aliyeinjinia dili la beki Fondoh Che Malone aliyefanya naye kazi Msimbazi iliyomsajili misimu miwili iliyopita akitokea CotonSport ya Cameroon na kugeuka kuwa beki kiongozi katika safu ya wana Msimbazi kwa kipindi hicho.
Che Malone alitengeneza ukuta mgumu sambamba na Henock Inonga aliyetimka klabuni hapo na kutua FAR Rabat, lakini msimu wake wa mwisho alifanya kazi akishirikiana na Abdulrazack Hamza pamoja na Chamou Karaboue – ukuta ambao uliifanya Simba kuendelea kuwa imara na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
Mmoja wa marafiki wa Benchikha ameliambia Mwanaspoti kuondoka kwa Che Malone Msimbazi akitua USM Alger nyuma yake kuna mkono wa Benchikha ambaye anatajwa ndiye aliyesimamia shoo nzima hadi nyota huyo akasaini mkataba na timu hiyo.
“Kabla ya Benchikha kupewa nafasi ya kuwa kocha mkuu wa USM Alger alikuwa sehemu ya benchi la ufundi kama mshauri na ndiye aliyependekeza baadhi ya nyota kusajiliwa akiwemo Malone. Nafikiri ni kwa sababu amefanya kazi na mchezaji huyo,” amesema rafiki huyo wa Benchikha na kuongeza:
“Tangu msimu uliopita jina la Che Malone lilikuwa katika meza ya majadiliano – hii ni baada ya kupendekezwa na kocha mwenye historia nzuri na klabu ya USM Alger. Baada ya msimu kuisha majadiliano yalianza na hatimaye kumnasa.
“Nafikiri ni chaguo sahihi kwake na ni miongoni mwa makocha ambao wamekuwa na tabia ya kuhama na wachezaji wao pale wanapopata nafasi ya kuondoka kwenye timu. Nakumbuka alifanya hivyo baada ya kuondoka Simba akiondoka na Sadio Kanoute na wengine.”
Rafiki huyo amesema sasa Benchikha ndiye kocha mkuu wa USM Alger akijiunga na kikosi hicho kwa mara nyingine akiwa na kumbukumbu nzuri ya kuiongoza timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na kuipa taji la Super Cup.