SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetangaza litakuwa na mdahalo wa kiufundi juu ya mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 yanayoendelea Afrika Mashariki, kitakachofanyika jijini Nairobi, Kenya, kesho Jumatano.
Kikao hicho kitahusisha wanachama maalum wa Technical Study Group (TSG) wa CAF, ambao watajadili kwa kina mwenendo wa kiufundi wa mashindano hayo ya nane.
CAF imesema lengo la majadiliano hayo ni kutoa uchambuzi wa kina juu ya mbinu zilizotumika, mwenendo wa wachezaji na mwelekeo mpya wa kiufundi unaoibuka katika mashindano.
Miongoni mwa wajumbe watakaohudhuria ni Mark Fish kutoka Afrika Kusini, bingwa wa AFCON 1996 na beki wa zamani wa Orlando Pirates, Lazio na Bolton Wanderers.
Fish anatajwa kuwa na utaalamu mkubwa katika saikolojia ya wachezaji, uongozi na maendeleo ya vijana.
Pia atakuwepo Abraham Mebratu kutoka Ethiopia, mwalimu wa kiwango cha juu wa CAF na mshauri wa muda mrefu katika masuala ya kiufundi.
Amewahi kuwa kocha mkuu wa timu za taifa za Ethiopia na Yemen, pia Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Yemen.
Tanzania itawakilishwa na Oscar Rabson Mirambo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, mwenye leseni ya juu ya ukocha UEFA Pro.
Mirambo amekuwa mstari wa mbele kuboresha mfumo wa soka la vijana nchini, kusimamia elimu ya makocha na kuimarisha miundombinu ya maendeleo ya mchezo.
Kutoka Kenya, atakuwepo Michael Amenga Okoth, kocha na kiongozi wa muda mrefu wa soka, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF).