Chadema, Polisi Pwani wavutana kuhusu makada 10

Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikiendelea kudai wanachama wake 10 kushirikiliwa na Polisi mkoa Pwani, pasipo kutoa haki ya kuonana na mawikili wao, jeshi hilo limesisitiza waliokamatwa ni wahalifu si makada wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Chadema, imedai kuwa polisi liliwakamata wanachama wake sita jana Jumamosi Agosti 16, 2025 waliokuwa na kikao cha ndani Kibaha mkoani Pwani.

Miongoni waliokamatwa ni kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), jijini Dar es Salaam kuwa ni Pendo Msechu, Pendo Kyosi, Mary Mushi, Samson Mzambia, Focus Laurent na Alfred Bundala.

Hata hivyo, Agosti 17, 2025 polisi mkoani Pwani ilitoa taarifa kwa umma ikisema imewakamata watu 10 waliokuwa ukumbi wa Mwitongo Kibaha Mailimoja Shule wakipanga njama za kufanya uhalifu.

Leo Jumanne Agosti 19, 2025 Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia ametoa taarifa kwa umma, akidai polisi imewazuia makada kutoonana na mawakili wala ndugu zao.

“Tunalitaka jeshi la polisi kutoa ushirikiano kwa ndugu na jamaa na mawakili wetu ili kuhakikisha wanachama waliokamatwa  wanapata haki zao za msingi, kwa mujibu wa Katiba yetu, haki za kuwasiliana, kuonana na ndugu na jamaa na mawakili wao,”

“Chadema tunalitaka jeshi la polisi kutoa taarifa mara moja kuhusu wanachama wetu waliokamatwa na waposhikikiliwa na kuwapatia dhamana au kuwafikisha mahakamani,kama wanaona wana makosa yanayostahili kushtakiwa ili haki itendeke,”amesema Rupia.

Wakati Rupia akieleza hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema “Waulize wao (Chadema) walikutana nani? Maana mimi sijakamata mtu wa Chadema.Nimekamata wahalifu sawa brother (kaka), hiyo ya Chadema waambie wakamuulize mtu anayehusika na vyama vya siasa,”amesema Morcase.

Katika taarifa hiyo, Rupia amesisitiza kuwa haki ya wanachama wa chama hicho, haiwezi kuizuliwa na polisi badala yake jeshi hilo linapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda na kutekeleza kwa vitendo sheria za nchi.