Dk ‘Manguruwe’ afikisha siku 287 rumande, upelelezi bado

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe, amefikishwa siku 287 akiwa rumande kutokana na upelelezi wa kesi yake ya uhujumu uchumi, kutokamilika.

Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya pekee yake.

Lakini Mkondya yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha ambalo halina dhamana, huku John yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namna 31523 ya mwaka 2024.

Tangu siku hiyo hadi leo Jumanne, Agosti 19, 2025 Mkondya amefikisha siku 287, huku upelelezi wa kesi hiyo ukiwa haujakamilika.

Hata hivyo, leo Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama hiyo upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kasala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.

Hakimu Magutu alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, 2025 kwa kutajwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28,  19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Katika moja ya mashtaka hayo washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo.

Inadaiwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa Mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi cha Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha hizo.

Katika mashtaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa mkoani Dar es salaam kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.