Hizi hapa fursa za kiuchumi za uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Ukiacha mbilinge za kisiasa, vijembe na vituko katika majukwaa ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu, tukio hilo limebeba pia fursa za kiuchumi na biashara kwa wananchi.

Kwa mujibu wa wadau mbalimbali wa biashara, tukio la uchaguzi linapaswa kutazamwa kwa jicho mtambuka, kwani linabeba fursa za kiuchumi na kibiashara, ambazo zinaweza kuwakwamua watu.

Kuchapisha fulana, kusafirisha wananchi, huduma muhimu kama chakula, vinywaji na malazi ni fursa chache tu kati ya nyingi zinazotajwa na wadau wa biashara kuwa mara nyingi zinapatikana nyakati za uchaguzi.

Kauli hizo za wadau wa biashara zinakuja wakati ambao imebaki wiki moja kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kuanza, Agosti 28, mwaka huu.

Kampeni za uchaguzi mkuu huo wa madiwani, wabunge na Rais zitafanyika kwa siku 61, na Jumatano ya Oktoba 29, 2025, itakuwa siku ya kupiga kura.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumanne, Agosti 19, 2025, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Taifa, Hamis Livembe, amesema tayari baadhi ya wafanyabiashara wameshaanza kunufaika na fursa za kuchapisha fulana.

Sio fulana pekee, amesema wapo wanaochapisha vipeperushi vya kampeni, matangazo yatakayotumika wakati wa kampeni, na hata wasanifu watanufaika.

“Wagombea wa nafasi ya urais wanapopita mikoani kufanya kampeni, watalala mikoa husika, nyumba za wageni zitatumika, magari yatakodiwa, wanaofanya biashara za mafuta kwenye magari watauza, hoteli zitauza vyakula, kwa hiyo biashara itakuwa kubwa wakati huo,” amesema na kuongeza;

“Kwa wale wanaotengeneza vipeperushi vya wagombea wakati wa kampeni, wanaokodisha vyombo vya muziki na magari ya kampeni, huu ndio wakati wa kuanza kusaka fursa, kwani kampeni zimekaribia.”

Amesema kampeni mara nyingi zinahusisha mavazi ya vyama na yanayowanadi wagombea. “Fulana, kofia, vitenge, skafu na bendera, wajasiriamali wanaojishughulisha na uchapishaji na ushonaji wana nafasi nzuri ya kupata tenda,” amesema.

Kundi lingine alilotaja litanufaika kiuchumi kupitia uchaguzi mkuu ni vikundi vya kutoa ulinzi wa mikutano ya kampeni, vifaa vya wagombea au usimamizi wa umati wa watu.

Ukiacha harakati za kisiasa wakati wa kampeni, kuna fursa nyingi za kibiashara zinazofunguka nyakati hizo, kama inavyoelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Hamad Komboza.

Ameeleza kuwa kampeni zinahusisha mikutano ya hadhara inayohudhuriwa na makundi mbalimbali, wapo watakaohitaji huduma muhimu, ikiwemo chakula na vinywaji. Hizo ni fursa kwa wenyeji wa eneo husika.

“Kuna wananchi wanakwenda kuwasikiliza wagombea, watahitaji vyakula na vinjwaji. Haiwezekani waondoke uwanjani bila kunywa na kula, kwa hiyo, kwa wakazi wa maeneo husika wanaweza kuchangamkia fursa hizo,” ameeleza.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania, Chuki Shaaban, amesema sekta ya usafirishaji ndio itakayokuwa nguzo muhimu kwenye uchaguzi mkuu.

Mara nyingi, amesema, wadau wa usafirishaji hupata fursa ya kusafirisha maboksi na karatasi za kupigia kura kwenda mikoani, wilayani, na hatimaye ngazi za chini na usafiri utakaowezesha hilo ni malori.

“Hakuna gari ndogo itakayotumika kusafirisha maboksi ya kura, bali ni malori. Hii inatuonesha kwamba madereva na wamiliki wa malori ndio fursa yetu kwenye uchaguzi huu. Niwaombe madereva kutumia uaminifu wao kuepuka kutumika kusafirisha kura za wizi au kuharibu uchaguzi huu,” amesema.

Ukiacha usafirishaji, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi kwenye vyombo vya habari (Jowuta), Mussa Juma, amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kupata fedha kwa ajili ya kuripoti uchaguzi mkuu, hasa maeneo ya pembezoni mwa nchi.

“Ni wakati muafaka sasa, tumewezesha vyombo vya habari kuwa na uchumi wakati huu wa uchaguzi, ili wanapokwenda kuandika habari wafike hadi maeneo ya pembezoni wanakoishi wamasai na jamii zile ambazo hazifikiwa,” amesema.

Amesema imeshuhudiwa waandishi wakitumia magari ya wagombea na kudhalilishwa, lakini kujitegemea wakati wa kampeni watafanya kazi kwa uhuru mkubwa.

Mbali na hayo, amesema wagombea wanahitaji kujitangaza kupitia mabango, vipeperushi, redio za mitaa, pamoja na mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, TikTok na WhatsApp. Hii ni fursa nyingine kwa vyombo vya habari.

“Hii ni fursa kwa wabunifu wa maudhui, wapiga picha, waandishi wa habari, na wasambazaji wa matangazo kufanya biashara,” amesema.

Moja ya usafiri unaotumika zaidi ni bodaboda, ambao pia huhanikiza shughuli za kampeni. Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Taifa, Said Kagoma, amesema tayari wameanza kunufaika wakati huu wa uchaguzi, hasa kwa kuondolewa baadhi ya tozo.

“Mbali na tozo, wakati wa kampeni wapo wagombea wanakodi bodaboda kufuata msafara wake kwa makubaliano. Wapo pia wananchi wanaokwenda kwenye kampeni hizo za wagombea, na lazima watatumia bodaboda kwa wingi kufika wanapokwenda na kurudi, kwahiyo ni fursa kwetu kwenye uchaguzi huu,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi, Mwalimu Samson Sombi, amesema kwa ujumla kampeni za uchaguzi mkuu ni nyenzo muhimu ya uchumi inayochochea shughuli za biashara na kuongeza mzunguko wa fedha nchini.

“Wakati huu wa uchaguzi kuna faida kwa sekta mbalimbali, hasa biashara ndogo ndogo na huduma zinazohusiana na siasa, lakini mafanikio ya kibiashara katika kipindi hiki yanahitaji mipango mizuri, uelewa wa soko, na ubunifu wa kufanikisha mahitaji ya wagombea na wafuasi,” amesema.

Mbali na hilo, amesema vikundi vya bendi za muziki, ngoma, na wasanii wa kizazi kipya huajiriwa kutoa burudani kwenye kampeni. Aidha, amedokeza kuwa wasanii wanaweza kutunga nyimbo za kampeni au kutumbuiza kwenye mikutano.