Dar es Salaam. Watumiaji wa mtandao wa kijamii wa Instagram, wamekuwa wakipata masasisho mapya (new updates) kila baada ya muda, hali inayotajwa kama ubunifu wa wamiliki wa mtandao huo (Kampuni ya Meta) ili kuongeza hamasa kwa watumiaji wake.
Kwa sasa Instagram iko kwenye majaribio ya kipengele kipya kiitwacho ‘Picks’ kitakachowawezesha watumiaji kupata ama kugundua mambo yanayowavutia kwa pamoja na marafiki zao.
Kipengele hicho kitawawezesha watu kupata video za filamu, muziki, vipindi vya televisheni wanavyopenda na zaidi kuona ni rafiki gani kati ya marafiki zao wanaopenda vitu hivyo.
Ni siku kadhaa zimepita tangu mtandao huo uje na kipengele cha ramani ambacho mtumiaji anaweza kutuma mahali alipo (Share map) lengo ikiwa ni kuongeza ushiriki wa marafiki katika maudhui.
Pia, vipengele vingine vipya vilivyopo hadi sasa ni kushiriki mahali ulipo kwa usalama na marafiki unaowachagua kupitia ramani ya Instagram. Pia, kuna ‘Friends” tab in Reels’ ambayo unaweza kuona maudhui aliyotengeneza aliyo-like au (repost) rafiki yako pamoja na kuanza nao mazungumzo kwa urahisi.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao huo kama zilivyochapishwa katika tovuti yake na mitandao ya BBC, Indian Express na ABC News Instagram sasa itakuwa inakagua mambo unayoyapenda kisha kulinganisha ili kuona ni rafiki yako yupi na yeye anavutiwa na mambo hayo.
Kuhusu kipengele kipya cha ‘Picks’ Instagram mtandao kitakuwa kama njia mpya ya watumiaji kuungana na marafiki na wafuasi kwa ukaribu zaidi, ikitoa njia ya kuanzisha mazungumzo kuhusu mada zinazowavutia.
“Ili kuwasaidia watu kuungana na marafiki kuhusu mambo wanayogundua kwenye Instagram, tutapunguza ujumbe maradufu, kufanya maudhui yanayotumia kuwa ya maingiliano zaidi na ya kijamii, na kuchunguza njia mpya za kuungana na marafiki,” mkuu wa Instagram Adam Mosseri amesema.
Ingawa hakuna maelezo rasmi yaliyotolewa, kipengele hicho kinalingana na lengo la mkuu huyo wa Instagram kwamba ni sehemu ya kukuza ubunifu na kuunganisha watu.
“Mtumiaji wa Instagram Monica Samuel amesema wakati mwingine hapendezwi kila baada ya muda kusasisha mtandao huo anaona kama usumbufu.
Mwingine David Kyando amesema ni vizuri kwa kuwa inaonesha ubunifu walionao wamiliki jambo linaloendana na muda.