Jaji Mkuu akemea watuhumiwa kunyimwa dhamana

Dodoma. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju amekemea tabia ya baadhi ya mahakimu kuwanyima dhamana watuhumiwa ambao kesi zao zinadhaminika akisema kitendo hicho ni kiashiria cha kutaka rushwa.

Jaji Masaju amesema kesi yoyote ambayo inaangukia katika kifungu cha dhamana, ni muhimu watuhumiwa wakapewa siku hiyohiyo ili kukwepa msongamano magerezani na ataanza kulifuatilia jambo hilo mwenyewe.

Masaju ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 19, 2025 wakati akifungua mkutano wa menejimenti ya viongozi wa mikoa, wilaya na taasisi zinazounda chombo walichokiita utatu wa pamoja.

Utatu huo unaunganishwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ofisi ya Mwendesha Mashtaka nchini (NPS), Polisi na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za kulevya nchini (DCEA) ambao wamekutana jijini Dodoma kuweka mkakati wa pamoja.

Amesema kitendo hicho ni aibu inayotia doa chombo cha Mahakama, pia hupelekea kesi ambayo ingesikilizwa siku mbili inapangwa miaka minne huku Watanzania wakiendelea kuumizwa na wachache ambao wanatumia nafasi hiyo kuwanyima haki watu wengine.

“Kumnyima mtu dhamana kwa wakati unaofaa, kumwekea vikwazo asikate rufaa ama kumuweka polisi muda mrefu ni kinyume na sheria za nchi yetu, lazima Mahakama iwe chombo cha kukimbilia na mfano kwa hapa duniani, lakini ninavyoongeza leo hatuko hata kwenye 10 bora,” amesema Masaju.

Amewaagiza wanaotoa haki waache kuwa na upendeleo na kama watu hawajajiandaa kuwafikisha wenzao mahakamani waache, akitolea mfano wa tabia za kuwaachia watu mahakamani halafu muda huohuo wanakamatwa tena na kufunguliwa mashtaka bila kesi kusikilizwa.

“Ukimpeleka mtu mahakamani jitahidi kumfanya ajue kosa lake mapema hata kabla hajasimama mbele ya hakimu ili kusudi aanze utetezi, kama kosa linadhaminika mwambie hata kabla ya kusimama mahakamani naye ajipange, na kukiwa na pingamizi la dhamana lielezwe siku hiyohiyo siyo kusumbua watu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Masaju amezungumzia hadhi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kwamba haina maana sahihi na tayari amefanya mpango wa kupeleka sheria bungeni ili wakaondoe neno hilo na badala yake iitwe Mahakama ya mkoa ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kuwaandaa mahakimu wenye sifa za kuwa majaji.

Awali, Mwenyekiti wa Utatu huo ambaye ni Mkurugenzi wa Mashtaka, Slyvester Mwakitalu amesema umoja huo umekuwa ni nguzo imara kwao hasa katika kupambana na uhalifu ambao sasa hakuna anayeweza kujificha.

Mwakitalu amesema walikuwa na ushirikiano wa Taasisi tatu, lakini wameongeza moja na kufikia nne kitendo kinachosaidia angalau kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na wamefanikiwa kuimarisha mifumo ya kushughulikia wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Ramadhan Kingai amesema katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu, hawategemei kurekodi uhalifu wa namna yoyote badala yake vyombo vimejipanga kushughulikia matatizo kabla ya kutokea.

Kingai amesema ndani ya ushirikiano huo, hawategemei kupanga mikakati isiyotekelezeka badala yake kila litakalojadiliwa lazima liwe na njia ya utekelezaji kwa ushirikiano mkubwa na kila mtu lazima atimize wajibu wake ili Tanzania na wananchi wake wawe salama.